Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Proparco, Françoise Lombard, wakati alipotembelea Makao Makuu ya AFD jijini Paris, Ufaransa. Ujumbe wa Benki ya CRDB ulikutana na kampuni ya Proparco kujadili maeneo ya kimkakati ya ushirikiano na fursa za uwekezaji nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akiwa katika mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Kilimo na Teknolojia ya Chakula wa taasisi ya Business France, Laure Elsaesser wakati wa ziara yake nchini Ufaransa. Ujumbe wa Benki ya CRDB upo nchini Ufaransa kukutana na wadau mbalimbali ili kuendeleza uhusiano na kujadili fursa za uwekezaji nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa SH Biaugeaud, Emmanuel Vallantin Dulac, wakati wa mkutano wa kujadili fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo Tanzania. Ujumbe wa Benki ya CRDB upo nchini Ufaransa kukutana na wadau mbalimbali ili kuendeleza mahusiano na kujadili fursa za uwekezaji nchini.
Ujumbe wa Benki ya CRDB ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Nsekela (katikati), wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wakuu wa Societe Generale Group wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji wa Kibenki Afrika, Cathia Lawson (wa tatu kushoto). Ujumbe wa Benki ya CRDB upo nchini Ufaransa kukutana na wadau mbalimbali ili kuendeleza mahusiano na kujadili fursa za uwekezaji nchini.
Katika ziara yake ya kwanza ya kikazi nchini Kenya, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa ahadi alipokuwa akizungumza kwenye mkutano maalumu na viongozi wa sekta binafsi.
“Tunakwenda kufungua nchi, Kenya kuna Uhuru ikimaanisha uhuru wa kufanya biashara; Tanzania kuna Suluhu maana yake ni suluhu za vikwazo vya kibiashara, mpira sasa uko kwenye himaya yenu,” Rais Samia alisema huku akipigiwa makofi na jumuiya za wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania.
Ili sekta binafsi iweze kufanya kazi na kuleta ukuaji wa uchumi, sekta ya fedha ni moja ya njia muhimu ya kufikia huko. Miongoni mwa vikwazo vingi vinavyoikabili sekta binafsi katika nchi kama Tanzania ni mahali pa kupata mikopo nafuu ili kuwekeza kama mtaji.
"Mitaji ni moja ya changamoto kubwa inayozuia ukuaji wa biashara na hivyo kuathiri uwezo wetu wa kuzalisha na kuuza kwa ushindani katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kama vile Kenya," alisema Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Angelina Ngalula.
Sekta ya fedha nchini imeitikia vyema mageuzi ya biashara na kiuchumi ya Rais Samia. “Sisi kama sekta ya fedha tuna wajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza uchumi kwa kutoa fedha kwa sekta ya umma na binafsi," anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekele ambaye yuko ziarani nchini Ufaransa kukutana na washirika wake na wawekezaji ikiwamo Shirika la fedha la Proparco.
Nsekela ambaye anaongoza ujumbe wa benki hiyo, ameahidi kuimarisha utoaji wa mikopo kwa kuongeza kiasi cha fedha za mikopo kupitia uanzishwaji wa ushirikiano na taasisi za fedha za kimataifa kama vile Proparco na nyingine.
Benki ya CRDB ambayo kwa mara ya kwanza ilitia saini ya makubaliano ya ushirikiano na Proparco, kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ufaransa (AFD) linalojihusisha na ukopeshaji wa kibiashara, inataka kupanua wigo wa ushirikiano na taasisi hiyo yenye makao yake makuu jijini Paris.
Machi mwaka huu, Benki ya CRDB na Proparco zilisaini makubaliano ya zaidi ya Sh182 bilioni kwa ajili ya kuongeza uwezo wake wa kukopesha wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini.
Kiasi hicho kilikuwa katika mfumo wa dhamana ya mikopo ambapo tangu makubaliano hayo fedha hizo zimeelekezwa kufadhili wajasiriamali kulingana na ajenda ya ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuzingatia biashara zinazoongozwa na wanawake ambazo zinaanza kutengemaa kutokana na athari za mlipuko wa janga la Uviko-19.
Proparco, sehemu ya Agence Française de Developpement Group (AFD Group), hutoa ufadhili na usaidizi wa biashara kwa taasisi za kifedha barani Afrika, Asia, Amerika Kusini na Mashariki ya Kati. Baada ya kupata mafanikio makubwa kutoka katika ufadhili wa awali, Benki ya CRDB imeona kuna fursa zaidi ya kushirikiana.
Nsekela alisema majadiliano yao na Mkurugenzi Mtendaji wa Proparco, Françoise Lombard yalijikita katika kukuza uwezo wa Benki ya CRDB katika kufadhili sekta binafsi, kusaidia uwezeshaji wa wajasiriamali walioathirika na janga la Uviko-19, pamoja na kuziba pengo la ufadhili kwa wajasiriamali wanawake Tanzania, na Burundi ambapo benki hiyo ina kampuni tanzu.
“Tunafuraha kuimarisha ushirikiano wetu na Proparco yanayolenga kuwezesha maendeleo endelevu na shirikishi. Tuko tayari kuongeza ushirikiano wetu na kutumia utaalamu wetu kufikia ajenda kabambe ya kusaidia ukuaji wa watu wetu na uchumi kwa ujumla,” alibainisha Nsekela.
Nsekela alieleza kuwa baada ya miezi michache ya ushirikiano na Proparco, wamegundua kuwa kuna fursa nyingi kwa benki hiyo kukuza biashara yake na uchumi wa Tanzania. Alisema menejimenti yake ina imani kuwa ushirikiano huo utaongeza mtaji wa Benki ya CRDB hivyo kukuza ukwasi wake wa kutoa mikopo katika nyanja zote za uchumi.
"Sishangai kwamba wawekezaji wanataka kushiriki katika uchumi wa Tanzania kwani Rais wetu Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa katika kufungua uchumi wa nchi na kuhakikisha kuwa nchi inafikia malengo yake ya kiuchumi," aliongeza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya CRDB.
Akizungumzia kuhusu ushirikiano wa pande hizo mbili, Mkurugenzi Mtendaji wa Proparco, Françoise Lombard alisema “Ushirikiano kati ya taasisi za fedha ni muhimu katika kusaidia maendeleo ya sekta binafsi na ukuaji wa uchumi. Nimefurahishwa na utayari wa Benki ya CRDB kuongeza ushirikiano kwani inaonyesha nia yao ya kusaidia biashara na wajasiriamali Tanzania, ambayo inaendana na lengo la Proparco.”
Lombard aliongeza kuwa, pamoja na msaada wa kifedha, wamejadili kutoa msaada wa kitaalamu kwa Benki ya CRDB ili kuboresha mbinu za benki hiyo za utoaji mikopo na kusaidia ubunifu wa bidhaa na hivyo kuongeza thamani ya uwekezaji wa Proparco na Benki ya CRDB katika maendeleo ya Taifa.
Kwa mujibu wa Lamborda, Tanzania ina uwezo mkubwa wa kukua kiuchumi kwasababu ya eneo lake la kimkakati la kijiografia na wingi wa shughuli za kiuchumi. “Ukuaji unawezekana tu ikiwa taasisi za fedha zitakuwa tayari kufadhili sekta za uchumi. Benki ya CRDB imeonyesha nia ya dhati ya kuwa sehemu ya safari ya mabadiliko ya Tanzania.”
Nchini Ufaransa, ujumbe wa Benki ya CRDB pia ulikutana na taasisi za Serikali, benki na wafanyabiashara kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji nchini. Baadhi ya taasisi hizo ni; Business France Idara ya Biashara ya Ufaransa inayohusika na kusaidia maendeleo ya kimataifa ya uchumi wa Ufaransa, Bpifrance Benki ya Uwekezaji wa Umma, na SH Biaugeaud kampuni inayojishughulisha na usindikaji wa matunda na mbogamboga.
Benki ya CRDB, mwaka huu pekee imeingia mikataba ya mikopo na dhamana ya zaidi ya Sh500 bilioni na mashirika ya Proparco USAID na DFC, IFC, AfDB na AGF kusaidia biashara na SMEs nchini.
Juni mwaka huu Benki ya CRDB, Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na Shirika la Fedha la Maendeleo la Marekani (DFC) walitia saini mkataba wa kuwezesha mikopo ya Sh100 bilioni.
Ubia huo ulilenga kusaidia benki kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha kwa wanawake na vijana hasa katika sekta ya elimu na afya ambazo ndiyo zinayoongoza kuwa na wafanyabiashara wengi wa sekta isiyo rasmi Tanzania.
Benki ya CRDB pia iliingia mikataba na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Mfuko wa Dhamana ya Afrika kwa Dola za Kimarekani milioni 110 ili kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wafanyabiashara wadogo na wakati wanawake katikati ya mwaka huu.
Akizungumza wakati wa utiaji sahihi wa mkataba huo Mkurugenzi Mkuu wa AfDB Afrika Mashariki, Nnenna Nwabufo alisema mkataba huo utaiwezesha Benki ya CRDB kuwezesha kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati hususan wanawake.
Mwezi Julai mwaka huu Benki ya CRDB ilipata uwekezaji mpya kutoka katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa fedha kwa biashara ndogo na za kati Tanzania na Burundi.
Katika mkataba huo, IFC ilitoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 100 kwa Benki ya CRDB, nusu ya fedha hizo zikiwa fedha za ndani na mkopo wa Dola za Marekani milioni 5 kwa Benki ya CRDB Burundi kusaidia mikopo kwa wafanyabiashara wadogo. Asilimia 25 ya mkopo huo kwa Tanzania utatolewa kwa biashara zinazomilikiwa na wanawake.
Zaidi ya hayo mwaka huu pia, Benki ya CRDB ambayo ndiyo benki kubwa zaidi nchini ilifanikiwa kupata uwekezaji wa Dola za Kimarekani milioni 130 kutoka masoko ya kimataifa kwa kusaidiana nna Benki za Investec kutoka Afrika Kusini na Intesa Sanpaolo kutoka Italia.
Kiasi hicho kitatumika kutoa mitaji kwa sekta ya ushirika na wajasiriamali wadogo na wakati nchini ikijumuisha fedha za miradi na miundombinu inayohusishwa na biashara ya bidhaa.
Mwaka 2019, Benki ya CRDB ilikuwa benki ya kwanza binafsi ya kibiashara kuidhinishwa na UN GCF kama mtoaji wa huduma za kifedha katika ufadhili wa Ajenda ya Kijani ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kwa hatua hii Benki ya CRDB sasa inaweza kufadhili miradi mbalimbali ya kijani yenye thamani ya hadi Dola za Kimarekani milioni 250 kwa kila pendekezo la ufadhili wa mradi mmoja.
Mwaka jana Benki ya CRDB ilizindua kituo cha Dola za Kimarekani milioni 200 kwa ajili ya kufadhili miradi inayowezesha kukabiliana na mabadiliko ya tabinchi nchini kupitia mpango wake wa ufadhili wa mpango wa kijani unaoitwa Mpango wa Kusambaza Teknolojia ya Kukabiliana na na Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania (TACADTP). GCF iliidhinisha Dola za Kimarekani milioni 100 kusaidia mradi huo, huku Benki ya CRDB nayo ikitenga kiasi kama hicho cha fedha.
“Kama benki inayoongoza Tanzania, Benki ya CRDB inaendelea kutafuta fursa za biashara katika sekta za kimkakati zitakazoleta maendeleo yanayohitajika ili kukuza uchumi wa nchi. Ushirikiano huu utatusaidia kukuza shughuli zetu za utoaji mikopo na kuimarisha zaidi nafasi yetu kama benki kiongozi,” Nsekela alisema.
Benki ya CRDB ndiyo benki kubwa zaidi Tanzania, ikiwa na mizania yenye thamani ya zaidi ya Sh10 trilioni. Kwa mujibu wa taarifa yake ya fedha ya nusu mwaka, benki hiyo ndiyo inayoongoza kwa kufadhili uchumi wa Tanzania, ikiwa na mikopo ya zaidi ya Sh6 trilioni.
Benki ya CRDB imeorodheshwa miongoni mwa taasisi kumi bora na salama zaidi kuwekeza barani Afrika na Moody`s Investors Services. Moody's imeipa Benki ya CRDB daraja la "B1" ambao ndiyo daraja la juu zaidi kuwahi kushikiliwa na taasisi za fedha, kusini mwa Jangwa la Sahara. Hii imezivutia taasisi nyingi za fedha za kimataifa kushirikiana na Benki ya CRDB.
Post A Comment: