Na Christina Thomas, Morogoro
MTOTO mwenye umri wa miaka mitatu mkazi wa Kijiji cha kisauke kata ya mkambarani mkoani Morogoro amekutwa akiwa ametahiriwa na watu wasiojulikana akiwa amelala nyakati za usiku nyumbani kwao.
Akizungumzia tukio hilo mwenyekiti wa mtaa wa kisauke alipotembelea familia ya mama iliyokumbwa na tukio hilo amesema amesikitishwa na kitendo alichofanyiwa mtoto Nasri Zahora cha kutahiriwa na watu kwa nguvu za giza ambapo amesema kitendo hicho ni cha kikatili na hakipendezi katika jamii hiyo.
Pia amewaomba wananchi wa kijiji hicho kuacha kujihusisha na shughuli za ushirikina kwa sababu hazifai katika jamii.
Mwenyekiti huyo alisema tukio hilo lilifanyika mnamo Julai 27 wakati mtoto akiwa amelala na mama yake kitandani.
Akielezea tukio hilo mama mzazi wa mtoto aliyejeruhiwa Asha Selemani alisema ilipofika majira ya saa kumi alfajiri mtoto wake alilia sana kitendo kilichomfanya astuke na kumnyayua mtoto wake kutoka alipolala na kumbembeleza lakini mtoto aliendelea kulia.
Amesema kuwa ilipofika majira ya asubuhi aliamka na kuendelea na shughuli zake lakini bado alikuwa hajatambua nini kilichokuwa kimempata mtoto wake na ulipopita muda wa kawaida wa kuamka alimwita amke lakini mtoto alishindwa kuamka kwa haraka kama kawaida yake na alipoamka alienda kupata choo kidogo ndipo alianza kulia na alipomkagua alitambua kuwa mtoto huyo amefanyiwa tohara.
Hata Hivyo Mama huyo ameiomba Serikali kumpa msaada wa kumchunguza mtoto wake kufuatia tukio hilo kwani mpaka sasa bado hajaweza kumpeleka hospitali kwa sababu hana uwezo na ametengana na mzazi mwenzie .
Naye jirani wa mama huyo Zatia juma mkazi wa Kijiji Cha kisauke amesema tukio hilo limewasikitisha majirani wote kwani ni tukio la kwanza kutokea katika Kijiji chao ambapo amesema tukio hilo ni la kikatili na la aibu kutokea kijijini hapo na linaaibisha Kijiji chao na kuwaomba wananchi wote kuacha kujihusisha na vitendo vya ushirikina kwani siyo mzuri.
Post A Comment: