Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC), DKT. James mataragio akizungumza katika uzinduzi wa TPDC Marathon leo Agosti 29,2022 katika Ofisi za TPDC Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi akizungumza katika uzinduzi wa TPDC Marathon leo Agosti 29,2022 katika Ofisi za TPDC Jijini Dar es Salaam. Mratibu wa mbio hizo Bw.Fred Kwezi akizungumza katika uzinduzi wa TPDC Marathon leo Agosti 29,2022 katika Ofisi za TPDC Jijini Dar es Salaam.
********************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wamezindua mbio za hisani (TPDC Marathon) zenye lengo la kuchangia gharama za upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya moyo ambapo imebainishwa kuwa kuna watoto 511 wanasubiri upasuaji katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 29, 2022 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la maendeleo ya petroli Tanzania (TPDC), DKT. James mataragio amesema Malengo yao ni kusaidia na kuunga mkono juhudi za kuokoa maisha ya watanzania na kwa kuanzia mbio hizo ambapo watarajiwa kusaidia upasuaji wa watoto 50 wenye matatizo ya moyo.
"Tumelenga kusaidi Taasisi ya Jakaya kikwete (JKCI) na tumeamua kuunga mkono katika kuokoa maisha ya watanzania wenzetu ambapo baada ya kukamilika mbio hizi tunategemea kusaidia watoto 50 kwa kuanzia"
Aidha Dkt.Mataragio alisema kuwa Mbio hizo ni endelevu kwa kila mwaka hivyo amewaasa wananchi kushiriki kwa wingi kama sehemu ya mazoezi ili kulinda afya zao lakini pia kwa upande mwingne kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo.
"Mbio hizi ni za kila mwaka na tutakua tunaendelea kuchangia kwa kadri ambavyo tutakua tunafanikiwa hivyo wananchi wote washiriki katika mbio hizi ili kuweza kuwasaidia wananchi wenzetu kuokoa maisha yao".Amesema Dkt.Mataragio.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi alisema kila mwaka asilimia moja ya watoto milioni mbili wanaozaliwa nchini Tanzania sawa na watoto elfu ishirini huzaliwa na matatizo ya moyo na kati yao asilimia ishirini na tano sawa na watoto elfu tano wanafanyiwa upasuaji wa moyo katika taasisi ya jakaya kikwete.
"Fedha zitakazopatikana zitatumika kikamilifu kwa malengo yaliyokusudiwa lakini pia kwa siku hiyo kutakuwa na upimaji wa magonjwa wa moyo bure, utoaji wa chanjo UVIKO-19 na uchangiaji wa damu kwa hiyari". Amesema
Nae Mratibu wa mbio hizo Bw.Fred Kwezi aliwahakikishia washiriki wa mbio hizo kuwa kutakuwepo na huduma zote za kimichezo, kiusalama na kiafya na kuwa Usajili unafanyika kwa kupitia TPDC pamoja na waratibu wa mbio hizo ambao ni Goba Rose Runners.
Mbio hizo zenye kauli mbiu isemayo “kimbia kwa afya yako” zinatarajiwa kufanyika septemba 11 mwaka huu katika viwanja vya farasi oysterbay jijini dar es salaam huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa raisi mstaafu wa serikali ya awamu ya nne Mhe. Jakaya mrisho kikwete.
Post A Comment: