Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo (katikati) akitoa elimu kwa wananchi waliofika katika Mnada wa Dutwa Bariadi mkoani Simiyu.
Na Kadama Malunde
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na watoa huduma za mawasiliano ya simu wameendesha Kampeni ya Kwea Kidijitali iliyohusisha utoaji elimu kuhusu uhakiki usajili wa laini ya simu kwa kupiga *106#, Matumizi sahihi ya namba 100 matumizi ya namba 15040 endapo utapigiwa simu au kupata ujumbe wa kitapeli na Matumizi salama ya mtandao kwa ajili ya Maendeleo ya Uchumi.
Kampeni hiyo imefanyika leo Alhamisi Agosti 25,2022 katika Mnada wa Mifugo na bidhaa mbalimbali katika Mji Mdogo wa Dutwa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Francis Mihayo amesema Kampeni ya Kwea Kidijitali inalenga kuhamasisha wananchi kuhakiki usajili wa laini ya simu (SIM Card Verification) kwa kupiga *106#
“Ili kuhakiki namba zako za simu zilizosajiliwa kwa namba ya kitambulisho chako cha NIDA piga *106# na kama utabaini kuna namba zipo lakini hujazisajili toa taarifa kwa mtoa huduma wako wa huduma za mawasiliano ili wazuie namba hizo”,amesema Mhandisi Mihayo.
“Tumia namba 15040 endapo utapigiwa simu au kupata ujumbe wa kitapeli. Usitume pesa kwa mtu usiyemfahamu, hakiki Ujumbe na namba inayokutaka utume pesa kabla ya kufanya muamala na kumbuka Mawasiliano baina ya mteja wa huduma za mawasiliano ya simu na mtoa huduma wake ni kuptia namba 100 pekee”,ameeleza Mihayo.
Aidha Mhandisi Mihayo amewataka wananchi kuepuka maelekezo yanayotolewa kupitia namba binafsi kuhusiana na huduma za mawasiliano ya simu huku akiwashauri watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kufungua link wasizozifahamu.
“Udhalilishaji Mtandaoni ni kosa la jinai hivyo Usichapishe chochote kuhusu watu wengine bila ridhaa yao, Zuia (block) mtu yeyote anayetuma maoni ya kukusumbua, kukutishia au yasiyofaa kuhusu wewe na toa taarifa kwa jeshi la polisi iwapo utapata shambulio la mtandaoni…Acha, Kemea,Ripoti”,ameongeza.
Katika hatua nyingine Mihayo amesema matumizi salama ya mtandao yanachangia katika Maendeleo ya Uchumi akisisitiza kuwa Mtandao una fursa nyingi za biashara, elimu, kilimo, afya, ajira na ubunifu hivyo kuwataka wananchi wazitumie ili kujiletea maendeleo.
“Matumizi sahihi ya mtandao hurahisisha na kukuza biashara, Habari mpya za nyumbani, kimataifa, burudani na michezo zimo mtandaoni”,amesema.
“Dijitali imerahisisha utumaji barua, vifurushi na vipeto. Posta Kiganjani mwako; furahia! Dijitali/mitandao/TEHAMA imeongeza wigo wa ubunifu katika nyanja mbalimbali .TCRA kwa ushirikiano na COSTECH sasa tunakupa rasilimali za mawasiliano bure zitakazowezesha kukamilisha wazo lako la Ubunifu katika TEHAMA”,ameeleza.
Post A Comment: