Lishe bora kwa watoto wadogo ni suluhisho la udumavu kwa jamii kama afanyavyo mama huyu.
Na Abby Nkungu. Singida
SUALA la lishe duni kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano mkoani
Singida huenda likabaki historia baada ya takwimu kuonesha kuwa tatizo sugu la
udumavu kwa kundi hilo limepungua kwa asilimia 10 katika kipindi cha miaka
minane iliyopita.
Kulingana na taarifa ya Utafiti wa Kitaifa wa Afya na Demografia, kiwango cha
udumavu kwa watoto wa umri chini
ya miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 39 mwaka 2010 hadi asilimia 29 mwaka 2018.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick anasema kuwa
mafanikio hayo ni matokeo chanya ya
juhudi mbalimbali zinazofanywa na idara ya afya na wadau wengine katika
kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mama na mtoto ili kupunguza
tatizo la udumavu katika jamii.
“Kama unavyojua hivi sasa Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa
juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) iliyoanza
kutekelezwa Januari mwaka jana na inaendelea hadi mwaka 2026. Kwa hiyo, ni
matumaini yangu hali itakuwa nzuri zaidi kwa watoto wetu” alieleza Dk Ludovick.
Alisema kuwa chini ya Programu hiyo, kila mdau amekuwa akitimiza vyema
wajibu wake lengo likiwa ni kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya kwa
kuboresha mfumo jumuishi wa sekta mbalimbali; ikiwemo afya bora, lishe, malezi
yenye mwitikio, ulinzi na usalama na fursa za ujifunzaji wa awali kwa mtoto.
Dk Ludovick alisema kuwa pamoja na wadau wengine kutimiza vyema wajibu wao
kupitia Programu Jumuishi, Serikali nayo kwa upande wake imeongeza bajeti ya lishe kwa mtoto kwa kila halmashauri
kutoka 1,000/- kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi 1,239/- kwa 2021/2022.
Hata hivyo, alisema kuwa licha ya juhudi hizo kusaidia kupunguza udumavu,
bado kuna changamoto ya ukondefu wa watoto kwa asilimia 5.1 na uzito pungufu
kwa asilimia 18.2 suala ambalo idara ya afya mkoa inaendelea kulifanyia utafiti
juu ya sababu zake ili iweze kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti changamoto
hiyo.
Daktari bingwa Mshauri wa magonjwa ya wanawake na watoto katika hospitali
ya Rufaa ya mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani anasema pamoja na tafiti
kuendelea kufanyika, mara nyingi suala la udumavu, ukondefu na uzito pungufu ni
matokeo ya lishe duni na huleta homa za mara kwa mara kwa mtoto.
“Lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo na pia
hudumaza ukuaji wa kimwili, kiakili na hupunguza uwezo wa mtoto kufanya vizuri
shuleni na ufanisi wa kazi katika maisha ya utu uzima. Ndio maana msisitizo
mkubwa huwekwa kwenye lishe bora kwa mtoto katika siku 1,000 za mwanzo; yaani
tangu mimba kutungwa” alifafanua Dk Muttani.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na walezi
wanasema kuwa cha muhimu ni kwa wataalamu wa afya na lishe kuendelea
kutoa elimu kwa jamii; hususan Vijijini, juu ya umuhimu wa lishe bora hasa kwa
akinamama wajawazito, wanaonyonyesha na
watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
“Fikiria katika karne hii eti bado kuna watu vijijini wanaamini mama
mjamzito akila mayai atazaa mtoto asiyekuwa na nywele. Pia wanazuiwa kula maini
kwa imani mbalimbali za kienyeji. Elimu
bado inahitajika sana katika suala la lishe", alisema Patrick Mdachi Ofisa
Maendeleo ya jamii mstaafu na Mtafiti wa masuala ya mila na desturi katika
jamii.
Rehema Daniel mkazi wa Ginnery na Tatu Athumani mkazi wa Kibaoni mjini
Singida wanasema pamoja na elimu duni juu ya lishe bora, ugumu wa maisha bado ni
changamoto nyingine kwani baadhi ya vyakula bora na muhimu vinahitaji
rasilimali fedha ili kuvipata.
“Unapenda umnunulie mwanao maziwa ambayo lita moja ni kati ya 1,500/- na
2,000/-. Kwa mwezi lazima uwe na takriban 45,000/-. Hapo bado hujaweka angalau yai moja la 500/- kwa siku na vyakula
vingine kwani hata viazi lishe na matembele vinahitaji hela” alisema Rehema na
kuungwa mkono na Tatu, huku wakiisihi Serikali kuangalia suala la mfumko wa
bei.
Kwa mujibu wa Mganga mkuu wa mkoa Dk Ludovick, mbali na kutoa elimu ya lishe kwa jamii kupitia kamati za ngazi mbalimbali, mkoa wa Singida pia una vituo 99 vya kutolea huduma za matibabu ya utapiamlo mkali kwa watoto wenye ukondefu.
Post A Comment: