Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Nurdin Babu amewataka Wakuu wa Wilaya,wakurugenzi na viongozi wengine Mkoani humo kuwasilisha kwake orodha ya wananchi wanaohitaji msaada wa chakula ili waweze kusaidiwa na serikali.
Ametoa maagizo hayo leo Agosti 20.2022 wakati akiendelea na ziara yake ya kujitambulisha kwa viongozi pamoja na kuhamasisha ushiriki wa zoezi la sensa ya watu na makazi litakalo anza rasmi Agosti 23.2022 ambapo amekutana na wenyeviti wa vijiji na vitongoji wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi.
"Mwaka jana mvua ilichelewa kunyesha na baadhi ya maeneo yalikosa mvua kabisa na kupelekea mimea shambani kutokustawi na kutoa mavuno kama ilivyo tarajiwa,wapo wananchi wanauhitaji wa kusaidiwa chakula na tayari wilaya ya Mwanga wamesha tuma taarifa kwangu hivyo na wengine wanitumie taarifa ili msaada ushughulikiwe" alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha amewataadharisha wananchi wa mkoa huo kuendelea kutunza chakula kilichopo kwa kuwa na kiasi cha kupika badala ya kupika chakula kingi hadi kumwagwa ikiwa ni pamoja na watakao pata msaada wa chakula kama vile Mahindi kuacha tabia ya kutengenezea pombe za kienyeji.
"Watakao pata msaada wa chakula waache tabia ya kutengenezea pombe za kienyeji,wakitumie kwa afya ya familia na sivinginevyo" alisema Babu.
Aidha amewataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji kusaidiana na Makarani wa sensa kwa kuwafikisha kwenye kila kaya ili kila mtu ahesabiwe.
"Mkisha wafikisha makarani kwenye kaya kaeni pembeni wafanye mahojiano na mwenye kaya maana ni siri yao,wewe mwenyekiti wa kijiji au kitongoji kaa pembeni" alisisitiza Mhe.Babu
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Moshi Abbasi Kayanda amemuhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa kupata ushirikiano ili kumsaidia Rais Samia katika kutimiza adhima yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Post A Comment: