Na Englibert Kayombo WAF – Arusha.
Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesitisha matumizi ya fomu ya Bima ya Afya (NHIF) ya kununulia dawa nje ya kituo cha kutolea huduma za afya (FORM 2C) kwa Hospitali zote za Rufaa za Mikoa.
Waziri Ummy Mwalimu ametoa maelekezo hayo leo kupitia vyombo vya habari mara baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi na kuangalia hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Mkoa wa Arusha
"Kuanzia jana Wizara ya Afya imesitisha matumizi ya fomu ya Bima ya Afya ambayo mgonjwa akifika hapa Hospitali na hakuna dawa anaandikiwa ile fomu akanunue kwenye maduka binafsi ya dawa” amesema Waziri Ummy Mwalimu
Amesema sio kazi ya mgonjwa kutoka nje kwenda kutafuta dawa na kuwataka watendaji ndani ya Hospitali kuhakikisha dawa zipo na zinapatika wakati wote na endapo hazipo wachukue wajibu wa kwenda kuzitafuta na kumpa mgonjwa.
Waziri Ummy ametaja sababu nyingine iliyopelekea kuchukua maamuzi hayo ni udanganyifu mkubwa uliokuwa ukifanyika kati ya watumishi pamoja na ushirikiano na maduka ya dawa kuhujumu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
“Dawa zipo hospitalini lakini kwasababu duka la nje ni la Kwangu namwandikia mgonjwa dawa hazipo nenda nje ukachukue dawa” ametolea mfano Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amesema malekezo ya kusitisha matumizi ya Fomu 2C yalishaanza kutekelezwa na Hospitali za Umma ambapo Hospitali ya Rufaa ya Taifa Muhimbili pamoja na za Kanda zilisitisha matumizi ya Fomu 2C toka tarehe 1 Juni, 2022 na kuanzia Julai 1 mwaka huu Hospitali za Rufaa za Mikoa nazo zinatakiwa kusitisha matumizi ya Fomu 2C.
Waziri Ummy amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili mara baada ya kusitisha matumizi ya Fomu 2C mapato ya Bima ya Afya upande wa dawa yameongezeka kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 2 hadi 4 ambazo walikuwa wakikisanya kwa mwaka hadi kufikia makusanyo ya Shilingi Bilioni 10 hadi 14.
Waziri Ummy amekemea tabia ya udanganyifu inayofanywa na wamiliki wa maduka ya dawa kwa kushirikiana na wataalam wa hospitalini katika vitendo viovu vya kuhujumu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
“Kama umeanzisha duka la dawa kwa lengo la kupata wagonjwa wa NHIF sii sawa, kama ulikuwa haufanyi ujanja utaendelea kufanya biashara” Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa katika kila Watanzania 100 ni Watanzania 8 tuu ndio wenye kadi ya NHIF hivyo watanzani 92 bado watanunua dawa kwenye maduka binafsi.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Arusha Dkt. Alex Ernest amesema wamejipanga kuhakikisha wanatekeleza maagizo yaliyotolewa na kuacha matumizi ya form 2C.
Tumejiandaa na tuna dawa za kutosha tuna asilimia 95 ya dawa zote muhimu pia tuna duka letu la dawa hapa ndani ya Hospitali, hivyo tunawahakikishia wananchi watapata huduma zote hapa hapa Hospitalini.
Mama Materu ambaye ni mkazi wa Arusha na mwanachama wa NHIF amepongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na Wizara na kusema kuwa amekuwa akifika katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupata dawa za matibabu ya presha hivyo kuwepo kwa dawa ndani ya Hospitali kutwawaondolea usumbufu wananchi.
Post A Comment: