WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua daraja la mawe lenye urefu wa mita 30 na upana wa mita saba lililojengwa katika barabara ya Iguguno-Kikhonda-Kinampundu wilayani Mkalama na amewapongeza wahandisi kwa ubunifu na ubora, hivyo ameagiza wapewe kazi nyingine.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 16, 2022) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua daraja hilo lililojengwa kwa kutumia teknolojia rahisi ya mawe akiwa kwenye ziara yake mkoani Singida. Daraja hilo limegharimu shilingi milioni 102.

Waziri Mkuu amesema daraja hilo zuri na lenye ubora ni mkombozi kwa wananchi wa kijiji cha Lukomo na wana-Mkala kwa ujumla. “Nawapongeza wahandisi wa mkoa wa Singida kwa ubunifu huu wa ujenzi wa daraja hili la mawe mlilolijenga kwa ubora na kwa gharama nafuu.”

“Daraja hili hapa miaka yote tulishindwa kulijenga kwa sababu ya gharama, ilikuwa lazima tupate shilingi milioni 500 kumbe Mainjinia wetu kwa utalaam wao wanauwezo wa kujenga daraja la kudumu na kwa gharama nafuu. Kupitia vikao vyenu vya TARURA hii taaluma muifikishe kwa wahandisi wengine ili kila mmoja kwenye mkoa wake aitumie na kwa mtindo huu tutajenga madaraja kwa gharama nafuu.”

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Mkoa wa Singida Mhandisi David Tembo amesema ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya kazi zilizofanyika katika mkataba wa matengenezo ya muda maalumu ya barabara ya Mwando-Miganga-Kinandili yenye urefu wa kilomita 12.39, kazi zote zimegharimu kiasi cha fedha shilingi milioni 444.

Mhandisi Tembo amesema kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo kutasaidia kuondoa changamoto ya mawasiliano iliyokuwepo  kwa wananchi hasa kipindi cha mvua za masika pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa kata za Iguguno, Kikhonda na Kinyangiri.

“Gharama za ujenzi wa daraja hili ni nafuu ukilinganisha na madaraja ya zege na nondo. Kama daraja hili lililogharimu shilingi milioni 102 lingejengwa kwa kutumia zege na nondo lingegharimu kiasi cha shilingi milioni 550. Pia ujenzi wake unatumia muda mfupi.”

Baada ya ukaguzi wa daraja, Mheshimiwa Majaliwa amezindua Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama lililokamilika kwa asilimia 100. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu shilingi bilioni 1.33 bila ya VAT. Jengo hilo limejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).


Share To:

Post A Comment: