Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack akiongea na wafugaji na wakulima katika ziara aliyoifanya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki katika Kijiji cha Njinjo kilichopo Wilayani Kilwa, mkoani Lindi jana.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akiwasikiliza baadhi ya wakulima walioharibiwa mazao yao na mifugo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao mkoani Lindi jana.
Na Mbaraka Kambona, Lindi
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amemtaka Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Mhe. Zainab Telack kuhakikisha anawakamata Wafugaji wote wanaopiga
Wakulima na kulisha mifugo yao katika mashamba yenye mazao.
Ndaki alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kusikiliza na kutatua
migogoro ya Wafugaji na Wakulima aliyoifanya katika Wilaya za Kilwa na Liwale,
mkoani Lindi Julai 2, 2022.
Alisema kuwa wafugaji wengi hasa wanaohamahama kutafuta malisho ndio
wanaolalamikiwa na wakulima kuwa wao
ndio chanzo cha vurugu,wanawapiga
wakulima na kulisha mifugo yao kwa ubabe katika mashamba ya wakulima
hao.
Aliongeza kwa kusema kuwa vitendo vya ubabe vinavyofanywa na baadhi ya
wafugaji havikubaliki, huku akisisitiza kuwa nchi haiwezi kuwa na jamii ya
namna hiyo, na hivyo wale wote wanaofanya vitendo hivyo hawatavumiliwa.
"Sasa Mkuu wa Mkoa na timu yako naomba
wale wote wanaopiga na kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima
wakamatwe kuanzia leo hii wawekwe ndani na wafunguliwe mashtaka ili sheria
ichukue mkondo wake," alisema Ndaki.
Kufuatia maelekezo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Zainab Telack
alichukua hatua za haraka na kuwaelekeza
wakuu wa vituo vya Polisi katika Wilaya ya Kilwa na Liwale kuwakamata
wafugaji waliowapiga wakulima na apatiwe taarifa ya utekelezaji wake haraka.
"Yupo kijana alimpiga diwani hapa Kata ya Kimambi na amemlipa laki
tatu na nusu (350, 000), nasema hiyo ni dharau na haikubaliki, nakuagiza OCD
upo hapa nataka uondoke na huyo aliyemlipa diwani, na wale wote wanaohusika na
vitendo hivyo wakamatwe leo ," alisisitiza.
Aliongeza kwa kusema kuwa wafugaji wote walioingia bila utaratibu mkoani
humo waanze kuondoka wenyewe kabla hawajaanza kushughulikiwa kwa sababu wao
ndio chanzo cha vurugu.
"Afisa mifugo na mtendaji wa kata nataka kuona wafugaji wote
walioingia kinyemela wanaanza kuondoka, na wafugaji wengine mnaobaki
mkiendekeza vitendo hivi nataka niwahakikishie nitawaondoa mmoja baada ya
mwingine," alifafanua.
Mmoja wa Wafugaji Wilayani Kilwa, Kidole Hababa alisema ili vitendo hivyo
viweze kukomeshwa ni muhimu Serikali ikawaita Wazee wa Wafugaji ili washirikiane nao kwa sababu
wazee hao wanawafahamu vijana wanaofanya vitendo hivyo watatumia njia zao za
kimila kuwawajibisha.
Aidha, katika hatua nyingi, Waziri Ndaki aliwataka Wafugaji kushiriki kikamilifu
katika zoezi la kusajili mifugo yao huku akiwahimiza kuanza kumiliki maeneo yao
ya kufugia akiamini kuwa wakifanya hivyo itasaidia kupunguza migogoro kwa kiasi
kikubwa.
Halikadhalika alitumia fursa hiyo pia kuwataka Watendaji wa Kata na Wenyekiti wa vijiji kujitafakari kwa sababu baadhi yao wanalalamikiwa kuwa sio waadilifu na kuwa ni sehemu ya migogoro hiyo.
Post A Comment: