Timu ya Mlalo FC imeibuka kidedea kwa goli 1-0 dhidi ya timu ya Shume FC zote za Mlalo Wilayani Lushoto mkoa wa Tanga katika fainali ya mashindano ya ligi ya Shangazi Mlalo Jimbo Cup.

Akifunga mashindano hayo Julai 16, 2022 yaliyofanyika Mlalo wilayani Lushoto, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha sekta ya michezo nchini kwa kufanya mabadiliko makubwa katika miundombinu ya michezo nchini.

“Kuna mabadiliko makubwa sana katika michezo nchini, tumeanza kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo, kwenye nyasi bandia, tutashuka kwenye jezi na mipira. Kubwa zaidi wizara yetu inakuja na program ya “Mtaa kwa Mtaa” chini ya Waziri wetu Mhe, Mohamed Mchengerwa ambaye Mama amemwamini” amesema Naibu Waziri Gekul.

Mhe. Gekul amesema progamu hiyo itaibua vipaji kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa na kuwahakikishia Watanzania kuwa Mhe. Rais Samia ameagiza, hivyo kama Wizara yenye dhamana ya Michezo nchini hawapendi kushiriki kwenye michezo, wanahitaji ushindi.

Aidha, Naibu Waziri Gekul amempongeza Mbunge huyo kwa kuanzisha ligi ya wanawake huku akishuhudia juhudi kubwa zinazofanywa na timu za wanawake nchini ambao wamelitoa taifa kimasomaso ambapo Timu ya Wanawake chini ya miaka 17 Serengeti Girls wamefuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka huu nchini India.

Naibu Waziri Gekul ametumia fursa hiyo kuwaasa watoto wa kike kujihusisha na michezo kwa kuwa Serikali inawekeza kwenye michezo na vipaji vyao vitaonekana na hatimaye kupata ajira hatua itakayowasaidia kuboresha na kuimarisha maisha na uchumi wao. 

Ameongeza kuwa wana Mlalo wanajituma katika kujenga taifa kwa kuwa siyo wavivu wanafanya kazi, mazingira ni mazuri na wanamuunga mkono Mhe. Rais katika sekta ya michezo na vijana wana vipaji vya michezo na kusisitiza fainali hiyo imekuwa na mchezo mzuri wa kuvutia kutazama kutokana na vipaji vya vijana ambavyo vitawafikisha mbali kwenye mchezo wa soka. 


Ligi ya Shangazi Mlalo Jimbo Cup ya wilayani Lushoto ilianza kurindima Agosti 2021 kwa udhamini wa Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashid Shangazi ambapo mshindi wa kwanza amekabidhiwa kombe na kitita cha Sh. 1,000,000/= na medali kwa kila mchezaji na benchi la ufundi huku mshindi wa pili akijizolea kitita cha Sh. 500,000/= na medali kwa kila mchezaji na benchi la ufundi.




Share To:

Post A Comment: