Na Dotto Mwaibale, Singida
MAKALANI 216 wa Sensa ya Watu na Makazi kutoka halmashauri zote mkoani Singida wameanza kupewa mafunzo ambayo yatawafanya kuwa wakufunzi na mafunzo hayo wameanza kuyapata Julai 6, mwaka huu na wanatarajia kuhitimu Julai 26, 2022.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo, alisema mafunzo kwa makalani yatafanyika kwa siku 21 na kueleza mara watakapohitimu watakuwa wakufunzi ambao nao watakwenda kutoka mafunzo kwa makalani ambao wataanza kufundishwa Julai 29, mwaka huu.
Kipuyo alisema Mkoa wa Singida unatarajiwa kuwa na makalani na wakufunzi wa sensa 5,402 ambao usahili wao umeanza jana Julai 19, mwaka huu.
Umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni pamoja na kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa;
Taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida , Dorothy Mwaluko, amewataka makalani hao kwenda kufanya kazi hiyo kwa weledi na umakini huku wakizingatia kiapo cha utumishi wa umma ili zoezi la sensa liweze kufanyika kwa mafanikio makubwa mkoani hapa.
Alisema makalani na wakufunzi lazima watambue kuwa zoezi la sensa ni muhimu sana na linakwenda kuweka historia katika maisha yao hivyo wanatakiwa kulifanya kwa umakini wa hali ya juu ili takwimu za idadi ya watu ziwe sahahi kwa maendeleo ya nchi.
"Juzi tukiwa na Waziri Mkuu alikuwa anatuambia na kutusisitiza suala la uwajibikaji, kila mtu awajibike na nyie hapa mtawajibika kama wasimamizi, likiborongwa huko chini hatuanzi na wa chini tunaanza na wewe msimamizi," alisema.
Mwaluko aliongeza kuwa wakati makarani na wakufunzi hao watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao watakumbana na changamoto kadhaa hivi suala la uvumilivu ni muhimu kwani watakutana na watu wa aina tofauti na wenye tabia tofauti.
"Ni lazima mjifunze 'culture' na 'attitude' za watu wa Singida, utakwenda kumhoji mtu kumbe ana 'stress' zake kwa hiyo kinachotakiwa ni uvumilivu ili kufanikiwa," alisema.
Alisema zipo taarifa nyingine ambazo itakuwa ngumu kuzipata kutoka kwa wananchi watakaokuwa wanawahoji hivyo kinachohitajika ni kutumia mbinu mbadala ya namna kumuuliza mtu.
Post A Comment: