Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Mwandami, ambaye alikuwa mgeni rasmi akizungumza kwenye usiku huo wa Stara.
Usiku wa Stara ukiendelea.
Wanawake wakiwa kwenye usiku huo wa Stara.
Usiku wa Stara ukiendelea.
Qaswida ikipigwa kwenye usiku huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Singida limeweka mkakati
wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kukomesha vitendo vya
unyanyasaji wa kijinsia, ulawiti na ubakaji ambavyo vimeshika kasi mkoa huu.
Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akizungumza juzi katika usiku wa
Stara, alisema maadili yamezidi kuporomoka katika mkoa huu na kuufanya kuwa wa
kwanza katika matukio ya unyanyasaji wa kijinsia.
"Takwimu zinaonyesha masuala ya unyanyasaji wa kijinsia, ulawiti na
biashara ya binadamu mkoa wetu umetajwa kuongoza, hili sio jambo jema inauletea
sifa mbaya mkoa wetu," alisema.
Sheikh Nassoro alisema hivi sasa kumeibuka tukio la ubakaji kuanzia saa
11:00 hadi 12:00 jioni ambapo baadhi ya madereva wa bajaji wamekuwa wakibaka
wanawake na watoto wanapowachukua kama abiria kwenye vyombo vyao vya usafiri.
Alisema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo BAKWATA imekuwa
ikishirikiana na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa
ambapo kuna kitengo cha kushughulikia masuala ya kijinsia katika ofisi ya
sheikh wa Mkoa.
Aidha, Sheikh Nassoro alitangaza kupiga marufuku watoto kusafirishwa kwenda
nje ya mkoa huu kwa ajili ya kufanya kazi za ndani kwani vitendo hivyo ndivyo
vinachochea matukio ya unyanyasaji wa
kijinsia.
"Hivi sasa tumeweka utaratibu mtoto yeyote anayesafirishwa kutoka
Singida kwenda mikoa mingine au nje nchi ni lazima atambulishwe kupitia ofisi
ya BAKWATA mkoa ili kutunza taarifa zake ili hata akipata changamoto yoyote
anasaidiwa," alisema.
Naye Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi anayeshughulikia Dawati la Jinsia,
Damas Mwakisabwe, alisema matukio ya kulawiti, ubakaji na unyanyasaji wa
kijinsia yamekuwa janga kubwa katika Mkoa wa Singida.
Mwakisabwe alisema matukio haya yanatokea kutokana na wazazi kusahau
majukumu yao ya kuwalea watoto wao katika maadili na hivyo kujiingiza katika
vitendo vibaya.
"Zipo kesi nyingi za matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo Jeshi
la Polisi inapata na cha kushangaza matukio haya baadhi ya watoto wanafanyiwa
wakati mwingine na ndugu zao wa karibu," alisema.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph
Mwandami, ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kumekuwa na watoto wengi wa
mitaani na kwamba kuna haja kwa viongozi wa dini wakae upya na serikali
kuangalia sheria ya ndoa ili ifanyiwe marekebisho.
"Hili ongezeko la watoto wa mitaani ni changamoto na linasababishwa kuwepo kwa ongezeko la wanadoa yaani baba na mama kuachana na hivyo watoto kukosa mlezi," alisema.
Post A Comment: