Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru,mwalimu Zainab Makwinya akionyesha baadhi ya vigae vya sakafuni vitakavyo tumika katika Zahanati hiyo.
Muonekano wa jengo la Zahanati ya Kikatiti
Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru,mwalimu Zainab Makwinya akimuonyesha mjumbe wa kamati ya siasa Robert Kaseko,namna ujenzi unavyoendelea katika Zahanati ya kikatiti iliyopo Wilayani Arumeru Mashariki Mkoani Arusha
Mwandishi Wetu,Arusha
Zahanati ya Kikatiti iliyopo wilayani Arumeru Mashariki mkoani Arusha ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Hassan alitoa jumla ya kiasi cha sh,10 milioni oktoba mwaka Jana kuchochea ujenzi wake inataraji kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Rais Samia wakati akiwa njiani kuelekea mkoani Arusha alisimama eneo la Kikatiti na kisha kusikiliza changamoto ya kukwama kwa ujenzi wa zahanati hiyo tangu mwaka 2013 ambapo alichangia fedha hizo na kuagiza mara moja ujenzi uendelee.
Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi wa halmashauri ya Meru,Mwalimu Zainab Makwinya alisema kwamba baada ya Rais Samia kutoa fedha hizo wao kama halmashauri kupitia mapato ya ndani walitoa sh,10 milioni kusukuma ujenzi huo.
Mwalimu Zainab alisema kwamba kitendo cha Rais Samia kutoa fedha hizo kimewatia chachu ya kukamilisha ujenzi huo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
"Bila Rais Samia hii kazi ingeendelea kubaki ilivyo kwa kuwa tusimgefanya lolote toka mwaka 2013 ilikuwa imekwama hakika tunamshukuru Mheshimiwa Rais"alisema Mwalimu Zainab
Alisisitiza kwamba wamejitahidi kutafuta wadau wa maendeleo kupitia shirika la misaada la CTSI la nchini Korea na benki ya NMB ambapo kwa kiasi kikubwa wamewasaidia kukamilisha ujenzi huo.
Hatahivyo,alisema kuwa kwa kuwa eneo la zahanati hiyo wamelipima na ni kubwa hivyo wanaiomba serikali ibadilishe zahanati hiyo na kuwa kituo cha afya.
" Tumeongeza vyumba viwili chumba kimoja cha wakinamama wajawazito kupumzikia wakati wakisubiri kujifungua na kingine cha kujifungulia hivyo kazi tunatarajia kuikamilisha mwishoni mwa mwezi huu tungeomba hiki kiwe kituo cha afya na sio zahanati maana ni kubwa na ya kisasa"aliongeza Mwalimu Zainab
Naye katibu wa shirika la misaada la CTSI ,Justine Mwaisemba alisema kuwa wao kama wadau wa maendeleo wameamua kumuunga mkono Rais Samia kwa kukamilisha hatua zote za ujenzi wa zahanati hiyo.
Mwaisemba alisema kuwa mpaka Sasa shirika lao limeshatumia jumla ya zaidi ya kiasi cha sh,99 milioni na wanatarajia kuongeza fedha zaidi kwa kuwa kazi bado haijakamilika.
" Sisi tumeamua kumuunga mkono mheshimiwa Rais Samia kwani eneo la Kikatiti halina zahanati ni jambo jema watu wa hapa wakipata huduma ya afya kwa kuwa huu ujenzi ulikwama tangu mwaka 2013" alisema Mwaisemba
Mjumbe wa kamati ya siasa mkoani Arusha,Robert Kaseko kitendo cha Rais Samia kutoa sh,10 milioni kilikuwa ni chachu ya kuchochea ujenzi unaoendelea na kumwagia sifa kiongozi huyo kwamba ni mpenda maendeleo.
Kaseko,alisema kuwa kamati ya siasa mkoa wa Arusha imeridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru,Mwalimu Zainab kwa kuwa ni mfuatiliaji na msimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutuchagulia viongozi wapenda maendeleo kamati ya siasa mkoa wa Arusha hakika tumeridhishwa na kazi inayofanywa mkurugenzi kwa kufuatilia na kusimamia vyema miradi ya maendeleo" alisema Kaseko
Post A Comment: