Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kulia) akisaini kitabu cha mahudhurio ya Wageni alipotembelea banda la maonesho la Wizara ya Mifugo na Uvuvi  yaliyokuwa yakifanyika katika Viwanja vya Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Maonesho hayo yalikuwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake ni Juni 5, 2022. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Sekta ya Uvuvi,  Bw. Melton Kalinga. Wengine kushoto ni Maafisa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Sekta ya Uvuvi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akipatiwa maelezo kuhusu uandaaji na uhifadhi wa malisho ya mifugo na Afisa Mifugo Mkuu, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani (Sekta ya Mifugo), Bw. Deograsias Ruzangi alipotembelea banda la maonesho la Wizara ya Mifugo na Uvuvi  yaliyokuwa yakifanyika katika Viwanja vya Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) akiangalia sehemu ya zana za uvuvi alipotembelea banda la maonesho la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Viwanja vya Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Anayemuonesha ni Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Sekta ya Uvuvi, Bw. Melton Kalinga (wa kwanza kushoto).

 

Na Mbaraka Kambona, Dodoma


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka Wafugaji na Wavuvi nchini kuhifadhi mazingira kama njia pekee ya kuziwezesha sekta hizo za mifugo na uvuvi kuwa endelevu katika kujipatia kipato na kukuza pato la taifa.

Ndaki alitoa wito huo baada ya kutembelea mabanda katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma Mei 5, 2022.

Alisema shughuli za ufugaji na uvuvi zinauhusiano mkubwa na utunzaji na uhifadhi mazingira na ndio maana wizara inawasisitiza wafugaji na wavuvi kuendelea kuhifadhi mazingira ili kufanya malisho ya mifugo yaendelee kuwa mengi na mazalia ya samaki yaweze kuwa endelevu na kutoa mazao ya kutosha.

“Sisi wizara tunazuia kabisa wavuvi kufanya uvuvi katika matumbawe ambayo ndio kiwanda cha kuzalisha samaki ili tuendelee kuwa na uvuvi endelevu na wenye tija kwa taifa”, alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa ili mifugo iwe na ustawi inategemea uwepo wa malisho na maji ya kutosha na ndio maana wanahimiza wafugaji kutunza nyanda za malisho na vyanzo vya maji ili ufugaji uwe na faida kwa wafugaji na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, sekta ya Uvuvi, Melton Kalinga alisema utunzaji wa mazalia ya samaki ni muhimu kwa uvuvi endelevu lakini pia ni moja ya vivutio vikubwa kwenye sekta ya utalii nchini.

Naye, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mazingira, Sekta ya Mifugo, Yusuph Selenge alisema kuwa ni muhimu kuhifadhi mazingira kwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwani kufanya hivyo kunasaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi huku akiongeza kuwa ni muhimu wafugaji kuzuia mifugo yao kuzagaa hovyo kwa sababu ni chanzo cha uhalibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Balozi wa Mazingira nchini na Mwandishi wa Habari, Oliver Nyariga alisema ni muhimu kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya afya ya jamii na kuepusha magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababishwa na uharibifu wa mazingira.

Naye, Miss Udom mshindi wa tatu, Agnes Budeba aliwaomba wavuvi hususan wanaofanya shughuli zao katika ukanda wa ziwa Viktoria kuhakikisha wanafanya uvuvi endelevu na kujiepusha na uvuvi haramu ili shughuli za uvuvi ziwe na tija kwao na taifa kwa ujumla.

 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: