WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea tabia ya utiririshaji wa maji machafu na majitaka kutoka viwandani na kwenye migodi kwani inachangia kuhatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira.
“Hivi karibuni tumeshuhudia kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai, maeneo mengi ya vyanzo vya maji yameathirika kutokana na ukame wa mara kwa mara, uchafuzi wa mazingira unaotokana na majitaka na kemikali kutoka na shughuli za viwandani. Uchafuzi huu umeendelea kuongezeka kwa kasi nchini na kuathari maji, hewa na ardhi. Hali hii inahatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumapili, Juni 5, 2022) wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa yamefanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Kaulimbiu yake ni Tanzania ni moja tu, Tunza Mazingira.
Vilevile, amekemea tabia ya uchomaji miti, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji wa miti holela kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu.
“Kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira, ninaagiza Wizara na taasisi husika, pamoja na wananchi kwa ujumla, kuimarisha ushirikiano katika kukomesha uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu kote nchini. Ninawasihi wananchi tutoe ushirikiano wa kutosha kuhakikisha tunarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili katika maeneo yetu, hususan maeneo ambayo miti ya asili iko kwenye tishio la kutoweka. Tuwe walinzi wazuri wa mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho,” amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ametoa maagizo 15 kwa wizara, taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu uhifadhi wa mazingira nchini na kutaka yatekelezwe kikamilifu.
Akizungumza na washiriki wa maadhimisho hayo kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Fedha na Mipango inapaswa ihakikishe Mpango Kabambe wa Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira unakuwa sehemu ya vipaumbele vya bajeti vya kila mwaka kwa kipindi chote cha utekelezaji wake wa miaka 10.
Amesema Wizara za kisekta, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinapaswa zihakikishe Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira unajumuhishwa katika mipango na Bajeti zao, sambamba na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji Ofisi ya Makamu wa Rais.
Amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa zisimamie uboreshaji wa maeneo yaliyoharibiwa kwa kupata tena miti. “Kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ihakikishe maeneo yote yaliyoharibiwa yanarejeshwa kwa kupandwa miti upya na kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ihakikishe inatekeleza vema programu ya kitaifa ya upandaji miti 1,500,000 ili kuhakikisha nchi yetu inakuwa ya kijani,” amesisitiza.
Amezitaka wizara, taasisi, mashirika ya Serikali na binafsi yanayotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia au shughuli nyingine za uzalishaji zianze kutumia nishati mbadala na kwamba kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ihakikishe inadhibiti matukio ya uchomaji ovyo misitu.
Kuhusu tafiti za nishati mbadala na viumbe vamizi, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za nishati mbadala ili kuondokana na utegemezi wa nishati ya kuni na mkaa kwa kupikia. Vilevile, ametaka zifanyike tafiti za namna ya kuzuia na kudhibiti kuenea kwa viumbe vamizi vinavyochangia uharibifu wa mazingira nchini.
Kuhusu takataka, amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweke utaratibu wa kuhakikisha taka zinatenganishwa na zinakusanywa na zile zinazohusika na usimamizi wa mifereji ya maji ya mvua mijini kuhakikisha mifereji hiyo inasafishwa ili kupunguza matukio ya mafuriko.
Kuhusu misitu na uoto wa asili, Waziri Mkuu amesema kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ihakikishe maeneo yaliyotengwa kwa matumizi ya misitu ya mijini katika mamlaka zao hayabadilishwi matumizi wala kuvamiwa. “Sekta zinazohusika zihakikishe kuwa ardhi na uoto asili katika vyanzo vya maji, vilima na milima iliyo katika maeneo yao inalindwa na kuhifadhiwa ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kukauka kwa vyanzo hivyo vya maji,” ameongeza na kusisitiza kuwa vilima vinavyozunguka mji wa Dodoma vihifadhiwe.
Kuhusu kilimo cha umwagiliaji maji, Waziri Mkuu amezitaka sekta zinazohusika na usimamizi wa shughuli za umwagiliaji mashamba zihakikishe kunakuwepo matumizi sahihi ya maji yenye kuzingatia uhifadhi na ulinzi wa mazingira.
Kuhusu hifadhi za wanyamapori, Waziri Mkuu amezitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa hifadhi za wanyamapori zidhibiti matukio ya ajali za barabarani kwa wanyamapori, na pia zidhibiti shughuli za binadamu pamoja na uvamizi katika maeneo ya mapito ya wanyamapori (shoroba) ili kupunguza uharibifu wa mazao, mali na binadamu kupoteza maisha kutokana na kuwepo mwingiliano wa wanyama na binadamu.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamiu wa Rais anayeshughulikia mazingira, Dkt. Suleiman Jafo amesema ofisi yake imezindua mpango wa soma na mti ambapo kila mwanafunzi anapaswa kupanda mti mmoja.
“Tumezindua kampeni ya Soma na Mti ambapo wanafunzi milioni 14.5 kutoka shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu wameshiriki kwa kupanda mti mmoja mmoja.
Waziri Mkuu alizindua Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira na kutoa tuzo kwa Mabalozi wa Mazingira na viongozi wakuu watano akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Post A Comment: