Na Mathias Canal, WEST-Arusha


Serikali imesema itachukua na kuyafanyia kazi maoni yote yanayotolewa na wadau wa elimu kuhusu Mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 na mitaala ya elimu ili kufanya mageuzi makubwa ya elimu nchini yanayotarajiwa kufanyiwa maamuzi mwakani.

Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia ina vipaumbele saba vya Serikali kwenye sekta ya elimu ambavyo ni kufanya mapitio ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014; kuangalia sheria ili iendane na matakwa ya sera; Mapitio ya mitaala ya elimu; Kuangalia idadi ya waalimu, wakufunzi, na wahadhiri wanaohitajika; Ubora wa walimu, Wakufunzi, na Wahadhiri; Kuimarisha ujenzi wa Miundombinu; pamoja na Upatikanaji wa vitendea kazi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 6 Juni 2023 wakati akizindua programu ya kuimarisha ujifunzaji kwa wanafunzi wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST Primary Student learning) iliyofanyika katika shule ya Msingi Arusha.

Utekelezaji wa programu hiyo utakuwa wa miaka mitano kuanzia mwaka huu 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 na ina thamani ya Dola za Kimarekani milioni 500 ambazo ni sawa na takribani trilioni 1.15 za kitanzania. Afua zote nane nilizozitaja zitatekelezwa kwa utaratibu wa lipa kulingana na matokeo.

Waziri Mkenda amewataja watekelezaji wakuu wa Programu hiyo kuwa ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. 

Aidha, amesema kuwa baadhi ya shughuli zitatekelezwa na Taasisi za kielimu zikiwemo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) na Mamlaka za Serikali za Mitaa huku baadhi ya Wizara zikishirikishwa katika utekelezaji wa afua zinazoendana na kazi za msingi za Wizara husika.

Waziri Mkenda ameyataja Matokeo yanayotarajiwa kupatikana katika miaka mitano ya utekelezaji wa programu hiyo kuwa ni pamoja na Vyumba vya madarasa 12,000 kujengwa ambapo lengo ni kujenga angalau vyumba vya madarasa 3,000 kila mwaka kuanzia mwaka ujao wa fedha 2022/2023, 

"Shule 6,000 kutekeleza mpango wa shule salama; Vituo vya walimu/shule za msingi 800 kuwekewa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kujifunza na utoaji wa mafunzo endelevu kwa walimu; Madarasa 12,000 ya Elimu ya Awali kuboreshwa" Amekaririwa Prof Mkenda

Ameyataja matokeo mengine kuwa ni pamoja na Uandikishaji wa wanafunzi wa Elimu ya Awali kuongezeka; Kuimarika kwa utawala na usimamizi wa shule katika ngazi ya shule na kata; na Kuimarika kwa ubora na uwezo wa walimu katika ufundishaji kutokana na mafunzo ya walimu kazini.

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda amewakumbusha wananchi kuwa tarehe 23 mwezi wa nane ni siku ya Sensa ya Kitaifa ya watu na makazi hivyo kila mwananchi ajitokeze kuhesabiwa ili kusaidia Serikali katika kupanga mipango bora ya utoaji wa Elimu











Share To:

Post A Comment: