Tafiti zinaonesha kuwa upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama hupunguza zaidi ya asilimia hamsini ya magonjwa ya kuambukiza, hivyo kwa kutambua umuhimu huo wa maji kwa afya na maendeleo ya wananchi, Serikali ina jukumu la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema hayo leo tarehe 29 Juni, 2022 akifungua mafunzo ya bodi na menejimenti za Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira nchini, jijini Arusha.
Amesema maji yana umuhimu wa kipekee katika maendeleo ya binadamu; kiuchumi na kijamii ambapo upatikanaji wa majisafi, salama na yenye kutosheleza ni nyenzo muhimu katika kuongeza ubora wa maisha, kupunguza makali ya athari zinazotokana na umaskini na kuongeza kipato cha wananchi.
“Lengo kuu la kuanzishwa kwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira ni kuboresha utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika maeneo husika” Waziri Aweso amesema.
Ameongeza kuwa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira ni Taasisi za Serikali zinazojitegemea ambazo zilianzishwa mnamo mwaka 1997 kupitia akaunti maalum chini ya Sheria ya Mwaka 1961(Cap Ordiance 281 Misceleneous Ammendment ACT). Baadae ilitungwa Sheria Na. 12 ya Maji na Usafi wa Mazingira 2009 ambayo iliendelea kuzitambua mamlaka hizi.
Na hivi sasa Sheria Na. 5 ya Maji na Usafi wa Mazingira, ya mwaka 2019 ambayo pia imezitambua mamlaka hizo na kuboresha masuala mbalimbali kuziongezea ufanisi. Mamlaka hizi hutoa huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa, Wilaya, Miji Midogo na Mamlaka za Miradi ya Kitaifa.
Post A Comment: