Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amewataka Watanzania kuthamini bidhaa zinazotengenezwa nchini na wazawa ili kuwapa moyo wabunifu na kuinua uchumi wa nchi.
Ameyasema hayo Juni 10, 2022 Jijini Dodoma wakati alipomwakilisha Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufungua maonesho ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Amesema Watanzania wengi wako tayari kununua bidhaa toka nje kwa bei ya juu badala ya kununua bidhaa toka nchini ili kukuza uchumi wa wabunifu na nchi kwa ujumla.
"Tumekuwa importers wakubwa wa bidhaa kutoka nchi za wenzetu kuliko kuhamasisha kununua bidhaa zilizotengenezwa na Watanzania wenzetu. Ndugu zangu tusipobadilika na kuwa wazalendo wa kuthamini vyetu, hatuwezi kuikomboa nchi yetu," amesisitiza Mhe. Jafo.
Aidha Mhe. Jafo amezitaka taasisi na mashirika ya Serikali na yasiyo ya kiserikali, makampuni na watu binafsi kufungua milango kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wanaotoka vyuoni kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo ili kuwajengea ujuzi na umahiri.
"Niombe taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi tuweze kuwatumia vijana wanaozalishwa na vyuo vyetu kwa ajili ya kufanya mafunzo ya kupata uzoefu na umahiri katika kazi kupitia taasisi zetu," amesema Mhe. Jafo.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema kuwa Serikali imepanga kuanza kuwapatia mikopo wanafunzi wa vyuo vya ufundi ili kupata idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivi.
Pia Prof.Mkenda amewataka NACTVET kufanya uchunguzi katika vyuo vyote vya ufundi ikiwa ni pamoja na VETA ili kuhakikisha vijana wanaoandaliwa wanakidhi katika soko la ajira.
"Niwatake NACTVET mkafanye tracer study katika vyuo vyote vya ufundi ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapatiwa elimu ambayo itawasaidia katika soko la ajira. Wazazi wanalipa pesa kwa ajili ya kuwasomesha watoto wao ili walete mafanikio katika familia na nchi kwa ujumla," amesema Mhe. Mkenda.
Katika hatua nyingine Waziri Mkenda ameahidi kuwa Serikali itafanya mpango wa maonyesho hayo kufanyika upande wa Zanzibar ili kuendelea kudumisha Muungano.
Kaulimbiu ya maonesho hayo ni kuinua ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya nguvukazi mahiri Tanzania.
Post A Comment: