Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Dodoma (DWJ),kimerejesha matumaini ya wanafunzi wawili waliokata tamaa ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano kutokana na kushindwa kumudu mahitaji mbalimbali ya shule.


Wanafunzi hao ni Jumbe Mohammed Jumbe aliyepata ufaulu wa daraja la kwanza katika mtihani wa kidato cha nne na kupangiwa kwenda shule ya  Sekondari ya fufundi Tanga Tech, na Ikram Said aliyepata daraja la kwanza na kupangiwa shule ya Sekondari Tosamaganga iliyopo mkoani Iringa.


Akizungumza wakati akiwakabidhi mahitaji ya shule,Mwenyekiti wa DWJ Oliver Nyeriga amesema huo ni mwanzo wa kuwashika mkono watoto walioshindwa kumudu gharama za mahitaji ya shule.


"Sisi wanawake ni wazazi,tunajua umuhimu wa elimu kwa watoto wetu,na Serikali imetoa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita,hivyo sisi kwa nafasi yetu hatukubali kuona watoto wetu wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya kukosa mahitaji,na huu ni mwanzo tu lakini lengo letu ni kuwafikia watoto wengi zaidi kwa kadri tutakavyojaaliwa,"amesema mwenyekiti huyo.


Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Antony Mtaka amekitaka Chama hicho kuendelea kuwaibua wanafunzi ambao wameshindwa kuendelea na masomo Kutokana na Changamoto mbalimbali zinazo wakabili.


Mtaka amewataka wanafunzi hao wakasome kwa Juhudi,ili wakawe mfano wa kuigwa na kuwaasa wasijiingize Kwenye Makundi yasiyofaa.


"Mimi napenda sana Elimu na ni kipaumbele changu kwahiyo mnavyotoka hapa muende mkasome na tutakuwa tunafuatilia maendeleo yenu mkasome ili nanyi badae mkasaidie wengine "


"Tunapenda siku mmefanikiwa mkatoe vipaumbele kwa wengine siyo baada ya hapo tena Kila kitu mnaenda kuongozwa na watu ambao hawajui historia yenu ya maisha ilikuwaje na mkishafanikiwa ndio utaona ndugu watakavyokuja wengi" amesema Mtaka.


 Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dk Fatuma Mganga amekipongeza Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake Dodoma DWJ kwa dhamira ya dhati ya kujitoa Katika kuibua wanafunzi ambao ndoto zao za kuendelea na masomo zilishapotea.


"Niwapongeze kwa hatua hii (DWJ) lakini pia mkasome watoto wetu Ili nanyi mkishafanikiwa mkawa viongozi mkasaidie wengine ambao watakuwa na Mazingira kama haya ambayo mnayapitia ninyi sisi sote tumesoma kwa kusaidiwa" amesema Dkt Mganga


Kwa upande wao wanafunzi hao ambao wamefanikiwa Kupata msaada huo Jumbe Mohamed na Ikram Said wametoa shukrani zao za dhati kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kwa Chama Cha Waandishi wa Habari wanawake (DWJ) na wameahidi kwenda kusoma kwa bidii bila kuwaangusha.

Share To:

Post A Comment: