Na Thobias Mwanakatwe
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma
mkoani Mara kimesema makundi
yanayotengenezwa na baadhi ya viongozi ndio chanzo cha kutokea malumbano
yasio na tija kwenye uchaguzi unaoendelea ndani ya chama ngazi ya matawi.
Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Musoma, Abubakari Nyamakato, alisema
hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kufuatia taarifa zilizoripotiwa
kwenye vyombo vya habari kwamba Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma, Magiri
Benedictor anadaiwa kupigana ngumi na Katibu wa Wazazi wilaya, Zainabu David
wakati wa uchaguzi wa chama tawi la
Nyasho.
Nyamakato alisema kimsingi tukio hilo halikutokea bali limepikwa na baadhi
ya viongozi ambao wamekuwa vinara wa kutengeneza makundi ndani ya chama na
kuwajengea chuki wengine kutokana na hofu ya kuja kuangushwa katika uchaguzi
mkuu wa 2025.
"Katika Wilaya yetu hii viongozi wawili (anawataja majina) ndio
wamekuwa ni tatizo na mabingwa wa kutengeneza makundi ndani ya chama na hata
katika tukio hili la uchaguzi tawi la Nyasho wamehusika kutokana na maslahi yao
ya kisiasa," alisema.
Nyamakato alisema kilichojitokeza ni kwamba baada ya kutokea malumbano
yaliyotokana na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa tawi kuonekana sio wakazi wa
tawi la Nyasho jambo hilo lilipofika wilayani ilitolewa agizo uchaguzi katika tawi
hilo uahirishwe ili kuorodhesha upya wajumbe halali wa tawi ndipo uchaguzi
ufanyike.
"Kimsingi hakuna ugomvi wala kupigana Mwenyekiti na Katibu wa Wazazi
kilichotokea wajumbe walikuwa wanabishana baada ya kubainika kulikuwa na
wajumbe ambao sio wakazi wa tawi la Nyasho," alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kutokea malumbano hayo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya
ambaye ndiye msimamizi mkuu wa chama alifika eneo hilo na kuagiza uchaguzi
uahirishwe kwanza ili kuepusha vurugu zaidi zisitokee.
"Kudai kwamba Mwenyekiti wa CCM amepigana na Katibu wa Wazazi huku ni
kutaka kuchafua Mwenyekiti aonekane hafai kwasababu wapo viongozi waliojipanga
kutaka kumchafua ili malengo yao ya kisiasa yaweze kutimia," alisema.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Musoma, Magiri Benedictor, alisema yeye ni
mkongwe katika mambo ya siasa hivyo
kamwe hawezi kufanya tukio la kupigana na Katibu wa Wazazi wilaya na kwamba
kinachofanyika ni baadhi ya viongozi wasiompenda kutaka kumchafua kisiasa.
" Mimi katika uongozi wangu nimekuwa na misimamo isiyoyumba ambapo
katika kukiongoza chama nazingatia kanuni na taratibu za chama sasa hilo ndilo
linalowaumiza mahasimu wangu wa kisiasa na sasa wananitengenezea mizengwe
kunichafua," alisema.
Benedictor alisema kama kweli alihushika kumpiga Katibu wa Wazazi suala
hilo lingekuwa limefikishwa polisi lakini hadi sasa halijapelekwa kokote zaidi
ya kuandikwa kwenye vyombo vya habari.
Aliongeza kuwa pamoja na mipango michafu inayofanywa na mahasimu wake wa
kisiasa kumchafua haitamkatisha tamaa katika harakati zake za kukipigania chama
na kukiongoza katika maadili ili kiendelee kuwa kimbilio la wananchi katika
kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Post A Comment: