Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amesema uhuru wa kujiendesha ni kipimo muhimu cha maendeleo katika Nchi yoyote duniani.


Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo akiongea na Viongozi wa Matawi 27 ya Chama cha ACT Wazalendo Jmbo la Tumbe,  katika Kikao Maalum kilichofanyika ndani ya Ukumbi wa Mikutano wa BI AWENA jimboni hapo, uliopo katika kijiji cha Tangana, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.


Mheshimiwa Othman amesema kuwa kuwepo kwa mamlaka, uhuru wa kujiendesha na kutekeleza mambo katika nchi yoyote, hupelekea upatikanaji wa fursa muhimu za kuimarisha jamii, na hatimaye kusaidia utekelezaji wa mipango bora ikiwemo ya kujikwamua kiuchumi.


Mheshimiwa Othman ametolea mfano kwa kusema, "mathalan Zanzibar inakosa Mabilioni ya Fedha ambayo ingeliweza kufaidika nazo pindipo isingelikoseshwa fursa ya kuwa Mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA)".


Naye Kaimu Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Ndugu Ismail Jussa Ladhu, amesema kuwa kufuata kwa udhati nyayo za Marehemu Maalim Seif, ni kutekeleza kwa vitendo yale yote mema aliyoyahamasisha Kiongozi huyo Mwanaharakati, yakiwemo uadilifu, ukweli, upendo na kujitolea kwa moyo wote, kwaajili ya maslahi ya Nchi na watu wake.


"Maalim Seif hakuangalia tumbo lake bali aliangalia watu wake na nchi yake, na hii ndiyo khulka njema ya kiongozi bora ambayo hapana budi kuigeza" ameeleza Jussa.


Akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa majukumu, mbele ya Ujumbe wa Makamu Mwenyekiti, Mratibu wa ACT-Wazalendo Pemba, Ndugu Said Ali Mbarouk, amesema kuwa Chama hicho sasa kimekoleza harakati zake za kujiimarisha Kisiwani humo zikiwemo za Usajili wa Wanachama kwa Njia ya Kielektoniki, zinazojulikana kwa jina la "ACT KIGANJANI".


Katika muendelezo wa ziara yake, Mhe. Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, na Viongozi mbali mbali wa Chama ngazi ya Taifa, ameshiriki katika harakati tofauti za kichama zikiwemo kuweka Jiwe la Msingi katika Tawi la ACT-Wazalendo Chimba,  pamoja na kuzindua Barza ya "OTHMAN MASOUD" ya Tumbe Kiperani, zote ndani ya Wilaya ya Micheweni.




Kitengo cha Habari

Ofisi  ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

07/06/2022.

Share To:

Post A Comment: