Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman amesema kuwa ipo haja kwa wanajamii kupambana kwa pamoja katika harakati za kujiletea maendeleo ili kujikwamua kiuchumi.


Mhe. Othman ameyasema hayo leo akizungumza na Wanakikundi cha Wajasiriamali wa  Kuatika Minazi cha "FIKIRA NI NJEMA" alipowatembelea katika kitalu chao kiliyopo Kwale, Jimbo la Ziwani Mkoa wa Kusini Pemba.


Mhe othman amesema kutokana na ukosefu wa nafasi za ajira serikalini, ni vyema zinapotokea fursa za kujiajiri zikiwemo za ujasiriamali kujenga mshikamano na kuzichangamkia kwa pamoja kwa lengo la kuunga raslimali na hatimaye kuweza kuyamudu maisha.


Mheshimiwa Othman amebainisha miongoni mwa fursa hizo bora kuwa ni pamoja na uatikaji wa vitalu vya miche bora ya kilimo, huku akisisitiza wito wake kwamba raslimali ya wanyonge ni umoja.


Akisoma risala kwa niaba ya kikundi hicho kilichoanzishwa mnamo mwaka 2015, Msemaji wa Kikundi hicho Ndugu Said Bakar Hamad, amesema kikundi chao kimeamua kujikita katika uatikaji wa minazi ili kurudisha haiba na sambamba  kukidhi mahitaji makubwa ya zao hilo hapa Visiwani, ambapo hadi sasa wameshaatika takriban miche elfu tano (5000) ya minazi.


Mhe. Othman aliyeambatana na Mke wake Mama Zainab Kombo Shaib, ametembelea kikundi hicho akiwa katika Ziara yake ya Maalum kisiwani Pemba.



Kitengo cha Habari

Ofisi  ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

06/06/2022.

Share To:

Post A Comment: