Katika kutekeleza agenda 10/30 inayoongozwa na kaulimbiu ya Kilimo ni Biashara, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo likiwemo Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki (EAGC) wameandaa maonesho ya kilimo biashara katika mashamba mfano ya TARI Uyole.
Mgeni rasmi katika maonesho hayo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Comredi Juma Zuberi Homera.
Maonesho hayo alibeba kaulimbiu inayosema "Mageuzi ya Kilimo Biashara, Jiandae Kuhesabiwa kwa Mipango Endelevu".
Akitoa salami za TARI, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Dkt. Richard Kasuga, alimshukuru mgeni rasmi na uongozi wa mkoa wa Mbeya kwa kuweka kipaumbele kusaidia Utafiti hususan Kituo cha TARI Uyole. Alipongeza Serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na Wizara ya Kilimo chini ya Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe kwa kutenga fedha kwa ajili ya utafiti na kuzalisha mbegu bora. Dkt. Kasuga aliongeza kuwa katika mwaka 2021/22 Serikali iliitengea TARI shilingi bilioni 11 fedha za maendeleo kutoka takribani bilioni 7 mwaka 2020/21. Aidha, katika mwaka 2022/23 Serikali imeitengea TARI bilioni 41 fedha za maendeleo. Fedha hizo zitachangia ufikiwaji wa Agenda 10/30 kwa kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na kuendeleza utafiti wa kilimo.
Aidha wakati akitoa hotuba yake, mgeni rasmi Mheshimiwa Comredi Homera pamoja na kuwapongeza TARI, taasisi na wadau wengine walioshiriki katika kufanikisha maonesho ya kilimo biashara, pia alitoa wito kwa wakulima na wadau kuzingatia yafuatayo:
- kutumia mbegu bora
- kushirikiana na wataalam wa kilimo ili kupata utaalam wa uzalishaji wa mazao
- Taasisi ya huduma za kilimo zikiwemo Wakala wa pembejeo (mbolea, mbegu bora na viuatilifu) kuweka programu endelevu za upatikanaji wa pembejeo hizo.
- Wataalam wa kilimo waendelee kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbegu bora, mbolea na viuatilifu.
- kuongezea thamani ya mazao ili kuongezea kipato na faida.
Katika maonesho ya kilimo biashara, TARI ilitambulisha teknolojia za mazao ya nafaka (ngano, mahindi na ulezi), maharage, soya pareto, viazi mviringo, parachichi na uhandisi kilimo.
Taasisi na makampuni mengine yaliyoshiriki maonesho ya kilimo biashara ni Seed Co, Kibo Seed, Highland Seed Growers, Beula Seed, Agriseed, Mashamba and Tractor, Syngenta Tanzania, Agro Z, na Mosanto. Mengine ni YARA, Minjingu, Zam seed, Meru Agro, CORTEVA, MATI Uyole, TALIRI, Western Seed na PANNAR.
Wakati akimkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi wa TARI Uyole Dkt. Tulole L. Bucheyeki alisema, huu ni mwaka wa nne (4) mfululizo, maonesho ya kilimo Biashara yamekuwa yakiandaliwa kwa kushirikiana na Wadau ambapo imefanikisha kuwaunganisha wadau katika mnyororo wa thamani.
Dkt. Bucheyeki aliongeza kuwa, maonesho haya ni muhimu kwa sababu matokeo ya utafiti hayawezi kuleta tija inayokusudiwa bila kushirikisha wadau katika kuzisambaza teknolojia hizo.
Post A Comment: