Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, imeupokea ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo Mifugo na Maji kuhusu kuongeza tija na uzalishaji wa mbegu bora kupitia mashamba ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) leo tarehe 11 Juni, 2022 Jijini Arusha wakati Wajumbe wa Kamati hiyo walipotembelea shamba wa ASA la Ngalamtoni nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Naibu Waziri amewaambia Wanahabari katika mahojiano maalum mara baada ya kumalizika kwa ziara iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Christine Ishengoma ambapo amesema ushauri kuhusu kufunga mihundo mbinu ya umwagiliaji katika mashamba ya ASA pamoja na kujenga uzio ili kuzunguka mashamba yote ya Wakala wa Mbegu za Kilimo nchi nzima na kuhuishwa rasilimali watu (Mafundi) wa Wakala kwenye muundo wa utumishi ili waendelee kufanya kazi kwa tija na kujiamini.
Naibu Waziri Mavunde amesema maelekezo ya Kamati ni kuwa Mtendaji Mkuu wa ASA kutangaza zabuni mara moja ili kumpata mkandarasi atakayefanya kazi ya kufunga miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba yote ya Wakala.
“Lengo ni kufunga miundombinu katika mashamba yetu yote; Tutafunga miundombinu ya umwagiliaji wa mabomba ya juu (Center pivot irrigation system) na mabomba ya juu na yanayotembea (Lateral pivot irrigation system), lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na umwagiliaji wa muda wote katika mashamba yetu”. Alisema Naibu Waziri Mavunde.
Mavunde amesema maelekezo hayo yataanza kutekelezwa mara moja na kwamba Waziri wa Kilimo naye kwa upande wake alishatoa agizo hilo siku chache zilizopita na kwamba, muda si mrefu agizo hilo litatekelezwa.
Naibu Waziri Mavunde ameongeza kuwa inakadiliwa ifikapo mwaka 2050 nchi ya Tanzania itakuwa na jumla la Watu milioni 129.4. Idadi hiyo ya Watu inatakiwa iende sambamba na uzalishaji wa kutosha wa chakula licha ya eneo la kilimo kuwa linapungua.
“Hivi sasa tumejikita katika kuongeza maeneo zaidi ya uzalishaji wa mbegu bora; Hili ni eneo muhimu ambalo tunapaswa kulipa kipaumbele. Mkakati wetu ni kuzalisha mbegu bora kwa ajili ya uzalishaji wa ngano pamoja na alizeti ili kupunguza utegemezi, wa ngano na mafuta ya kula”. Amekaririwa Naibu Waziri Mavunde.
Wakati huo huo; Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kuisimamia na kuishauri Wizara ya Kilimo katika kutimiza malengo iliyojiwekea.
Aidha Naibu Waziri Mavunde amesema mkakati wa Serikali kuhakikisha nchi inajitosheleza katika uzalishaji wa mbegu bora.
“Nchi yoyote ambayo imepiga hatua katika Sekta ya Kilimo; Iliwekeza katika utafiti na uzalishaji wa mbegu bora”. Alisema Mavunde.
Naibu Waziri Mavunde amesema kuwa eneo la uzalishaji wa mbegu bora za Kilimo limeongezewa bajeti kutoka bilioni 10.5 mwaka 2022/2021 hadi bilioni 43 mwaka 2022/2023 ambapo lengo kupunguza utegemezi kwenye zao la ngano na alizeti kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya kula.
Post A Comment: