Serikali imesisitiza kuwa kinachoendelea katika eneo la Loliondo mkoani Arusha ni uwekaji wa alama za mipaka kama ilivyo kwenye maeneo mengine ya hifadhi hapa nchini.
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori katika wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Maurus Msuha amesema, lengo ni kutenganisha maeneo ambako shughuli za kibinadamu zinaendelea na kule ambako haziruhusiwi na kwamba hakuna mtu anahamishwa kutoka kwenye eneo hilo.
Dkt. Msuha amesema, katika wilaya ya Ngorongoro serikali inaendesha mazoezi mawili kwenye maeneo mawili tofauti na kila zoezi limepangwa kulingana na mahitaji ya eneo husika na hakuna muingiliano wowote.
Amesema kuwa katika eneo la pori tengefu la Loliondo, serikali inaweka mipaka kutenganisha eneo la kilomita za mraba 2,500 kwa ajili ya wananchi na kilomita za mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi wa eneo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa mfumo wa ikolojia ya hifadhi ya Serengeti.
Dkt. Msuha ameeleza kuwa serikali itaweka mpango bora wa matumizi ya ardhi ya eneo la Loliondo, ili kusitokee muingiliano baina ya maeneo ya wananchi na eneo la hifadhi.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka amebainisha kuwa taarifa zilizoripotiwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa kuna Ng’ombe wamekufa baada ya kuhamia Kijiji cha Msomera hazina ukweli na kueleza kuwa picha hizo ni za Ng’ombe waliokufa katika nchi ya Jirani kutokana na matatizo ya ukame mwaka 2018.
Ameongeza kuwa kuwa zoezi la wananchi wa Ngorongoro wanaohamia kwa hiari kwenda Msomera linaendelea vizuri na wananchi wameendelea kuhamaiska na kujitokeza kujiandikisha, aidha kundi la tatu la wanachi wa Ngorongoro lenye kaya zaidi ya 25 linatarajiwa kuhamia msomera siku ya alhamis ya wiki hii.
Ngorongoro na Loliondo ni sehemu mbili tofauti zilizohifadhiwa na Serikali ambapo Loliondo ni eneo linalowekwa alama za mipaka ili kutofautisha shughuli za uhifadhi na maeneo ya wananchi.
Aidha zoezi linalofanyika katika Hifadhi ya Ngorongoro ni jambo la hiari linalohusisha wananchi kuhama kwa hiari yao wenyewe kwenda Kijiji cha Msomera Mkoani Tanga ambapo Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wananchi hao.
Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Tanzania Dkt. Maurus Msuha akifafanua jambo wakati akiwasilisha mada kuhusu zoezi la uwekaji wa alama katika pori tengefu la Loliondo na zoezi la Wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera Handeni Mkoani Tanga,kwenye kikao na Waandishi wa Habari kilichofanyika jijini Arusha tarehe 29 Juni, 2022.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka akizungumza kwenye kikao Maalimu na Waandishi wa Habari kilichofanyika jijini Arusha tarehe 29 Juni, 2022,akieleza kuhusu taarifa zilizoripotiwa kupitia mitandao ya kijamii kuwa kuna Ng’ombe wamekufa baada ya kuhamia Kijiji cha Msomera ambazo hazina ukweli na kueleza kuwa picha hizo ni za Ng’ombe waliokufa katika nchi ya Jirani kutokana na matatizo ya ukame mwaka 2018.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia yaliyokuwa yakielezwa kwenye mkutano huo maalumu.
Post A Comment: