Julieth Ngarabali, Kibaha.
Serikali Mkoani Pwani imekabidhi pikipiki tisa katika Halmashauri zake zote kwa ajili ya Maafisa ushirika kuzitumia kufanya shughuli za usimamizi na ukaguzi wa vyama vya Ushirika hatua ambayo imetajwa itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya usimamizi uliokuwa unatokana na ukosefu wa vifaa.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amekabidhi pikipiki hizo zilizotolewa na Tume ya maendeleo ya Ushirika nchini kwa maafisa Ushirika hao na kusisitiza kuwa wataalamu hao hawatapimwa kwa taarifa zao za wanakotembelea ni maeneo gani bali watapimwa sana kwa kuona ufanisi katika kazi wanazozisimamia katika kila Halmashauri.
"Leo ninawakabidni pikipiki tisa kwa niaba ya Serikali ikiwa ni sehemu za jitihada za Serikali kuweza kuboresha kilimo nchini na Mkoani Pwani ambapo inalimwa mazao kwa ajili ya chakula na biashara kwa hiyo hatutawapima sana kwa taarifa zao za wametembelea maeneo gani bali tutawapima sana kwa kuona ufanisi katika kazi wanazozisimamia "amesema Kunenge na kuongeza
" tukiona migogoro katika vyama vya ushirika vinaendeshwa vizuri,tukiona ufuta na korosho za wananchi hazipotei katika maghala ,tukiona usimamizi wa malipo na ugawaji pembejeo na tija tutajua kwamba kweli wanafanya kazi iliyonzuri"
Kunenge ameongeza kuwa kilimo na ushirika unaosimamiwa na Maafisa hao unagusa maisha ya wananchi wa ngazi za mwanzo wenye uwezo mdogo kwa hiyo kwa kupewa vitendea kazi hivyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amewagusa moja kwa moja raia wa kawaida kabisa wenye uwezo mdogo na maisha ya kawaida
Awali Mrajisi Msaidizi Mkoani Pwani Angela Nalimi katika taarifa yake ameeleza changamoto katika usimamizi wa shughuli za Ushirika ni pamoja na idadi ndogo ya maafisa ushirika ukilinganisha na maeneo ya utawala, uhaba wa vitendea kazi rasilimali fedha ,usafiri na vifaa na ukosefu wa elimu ya ushirika kwenye jamii.
Ingine ni ukosefu wa maghala bora ya kuhifadhia mazao hali inayopunguza ufanisi wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani na baadhi ya viongozi na watendaji wa ushirika kutokua waaminifu hivyo kufanha hujuma mbalimbali dhidi ya mali ya ushirika na kupunguza imani ya watu kwenye ushirika.
Aidha ametaja mikakati ya kuimarisha ushirika katika Mkoa huo ni kusimamia maagizo ya Serikali yanayoelekeza ununuzi wa mazao ya kimkakati kupitia vyama vya ushirika vya mazao jambo ambalo litaimarisha vyama vya ushirika, kusimamia mfumo wa stakabadhi ghalani ili kupata bei nzuri kwa mazao ya wakulima na hivyo kuwaimarisha kiuchumi.
Katika hatua ingine Nalimi ameeleza mafanikio yaliyoanza kupatikana kupitia zao la ufuta mkoani Pwani kuwo tayari wameua tani 6,500 za ufuta na wameshaingiza zaidi ya sh. 18 Bilioni kwenye minada miwili tu iliyofanyika ya uuzaji zao hilo na kwamba zoezi la kuuza linaendelea kwa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.
Nao maafisa Ushirika hao waliopewa pikipiki hizo wameishukuru Serikali kuwapatia pikipiki hizo kwani itawasaidia kuhudumia maeneo ya pembezoni kwa ufanisi na tija zaidi.
"Mfano Halmashauri ya Chalinze ina kata 15 kuna maeneo mengine ni mbali kutoka makao makuu ya Wilaya ni kilomita zaidi ya 100 kama kata ya Kibindu, Kimange na Mbwewe hivyo pikipiki hii itasaidia sana na kwa niaba ya wenzangu tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutukumbuka na sisi"amesema Raphael Kajale Afisa ushirika Chalinze
Mwisho.
Post A Comment: