Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Eliamani Sedoyeka amewataka Wathibiti Ubora wa Shule nchini kufuatilia na kusimamia uwajibikaji wa Wakuu wa Shule kwenye  fedha za miradi ya ujenzi wa shule zilizopelekwa na Serikali katika maeneo yao.


Amesema hayo Jijini Dodoma wakati wa kufunga kikaokazi cha Viongozi, Maafisa Uthibiti Ubora wa Shule Makao Makuu na Wathibiti Ubora wa Shule Kanda na Wilaya Tanzania Bara.


Amesema kuna ujenzi wa miundombinu ya shule unaendelea ikiwemo kupitia Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo amewataka kuhakikisha wanashiriki usimamizi wake na kutoa ushauri katika kuzingatia vigezo vya ubora vinavyohitajika  kulingana na miongozo na Sera.


Amesema wathibiti ubora wa shule wanaweza kuisaidia Serikali katika kuhakikisha elimu bora yenye kuwasaidia vijana kupata maarifa, stadi na ujuzi inapatikana kwa kukagua vyema shule na vyuo vya ualimu.


Sedoyeka ameongeza kuwa Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika idara hiyo ikitambua kuwa wathibiti ubora ni mboni ya jicho ya elimu na amewahimiza wakasimamie ubora wa elimu kwa kuwa matokeo ya uthibiti ubora ni kuwepo kwa elimu bora huku akisisitiza suala la kuzingatia matumizi ya TEHAMAkatika utendaji.


"Ni wakati muafaka kufikiria ni namna gani mnaweza kuzifikia shule hata bila kufika hata kwa kutumia maafisa elimu kata ili kufanya ufuatiliaji," amesema Prof. Sedoyeka.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Uthibiti Ubora upande wa Ualimu, Mathias Mvula amemweleza Katibu Mkuu kuwa kikao hicho kimekuwa na tija kwa kuwa wamepata fursa ya kufanya tafakari ya pamoja kuona yale waliyoyapanga kama yametekelezeka na kupanga mikakati ya utendaji ili kuongeza ufanisi.


Akizungumza kwa niaba ya Wathibiti ubora hao,  Amon Lembao kutoka Kanda ya Kati, amemshukuru Katibu Mkuu Sedoyeka kwa kuwezesha kikao hicho kwa kuwa mada zilizotolewa zimewapatia mahiri mbalimbali zitakazokwenda kuwasaidia katika utendaji.

Share To:

Post A Comment: