Watafiti wa Mradi wa Rise (Reserch on Improving Systems of Education) leo tarehe 09/06/2022 wamewasilisha matokeo ya tafiti walizozifanya kwa muda wa miaka minne katika Mkutano wa Nne wa Kundi la wadau linalojumuisha wajumbe kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wadau wa Maendeleo, Asasi za Kiraia na Taasisi za Umma na Binafsi.
Mradi huo wenye lengo la kutafiti namna ya kuboresha mifumo ya Elimu nchini unawashirikisha watafiti kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Elimu Tanzania na Chuo Kikuu cha Georgetown kilichopo nchini Marekani.
Kikao hicho kilifunguliwa na kuendeshwa na Wenyeviti wenza, Prof Carolyne Nombo ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Dkt.Charles Msonde Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Katika ufunguzi wa kikao hicho cha uwasilishaji wa matokeo ya tafiti Prof.Carolyne Nombo amesema matokeo ya tafiti hizo yatasaidia katika mapitio yanayoendelea ya sera na mitaala ya Elimu Tanzania.
"Nawapongeza watafiti wote na matokeo haya yamekuja kwa muda muafaka ambapo wote tunajua kwa sasa nchi yetu ipo katika mapitio na maboresho ya Sera na Mitaala ya Elimu,natumaini matokeo hayo yatasaidia sana kuonesha mahitaji ya uboreshaji". amesema Prof.Nombo.
Kwa upande wake Dkt. Msonde amewapongeza watafiti na kusema kuwa, utafiti huo umekuja wakati muafaka na kuwa utaisadia wizara kufanya maamuzi yanayoongozwa na matokeo ya utafiti.
“Ni mategemeo yangu kuwa matokeo ya tafiti yatakayo wasilishwa leo yatasaidia katika kutoa maamuzi katika mijadala ya kisera na katika kupanga namna bora ya kuanzisha na kusimamia miradi ya kielimu.”amesema Dkt.Msonde.
Akieleza lengo la Mkutano huo Dkt.Aneth Komba Mkurugenzi Mkuu TET na mmoja wa watafiti wa RISE amesema kuwa mradi huo ulianza Mwaka 2018 na unatarajia kumalizika mwezi Oktoba, 2022 ukiwa unatekelezwa katika nchi za Tanzania, Ethiopia, India, Vietnam, Nigeria, Indonesia na Pakistan.
Aidha ameeleza kuwa kwa upande wa Tanzania watafiti wa RISE wamefanya jumla ya tafiti 16 katika maeneo makuu matano ambayo ni Mabadiliko ya Mitaala, Mfumo wa uthibiti ubora wa shule, Mafunzo kwa walimu, Motisha kwa walimu na mifumo ya kiutawala katika elimu.
Ameongeza kuwa wanatarajia kuwa matokeo ya tafiti hizi yataweza kuisaidia Serikali katika kufikia malengo ya kutoa Elimu bora kwa kila mtoto.
Naye Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Georgetown Prof. James Habyariman amewashukuru sana wajumbe wa mkutano huu kwa maoni yao na mapokeo ya matokeo ya tafiti zilizowasilishwa.
Aidha amezishukuru wizara hizo mbili kwa kusimamia uendeshaji wa mikutano ya aina hii na kuchangia katika agenda zote za utafiti wa RISE tangu mwaka 2018.
Prof Habyariman ameahidi kuishirikisha wizara husika matokeo ya tafiti zote ili wizara ziangalie namna bora ya kutumia mapendekezo kutoka katika tafiti hizi.
Post A Comment: