Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Mulagiri (wa pili kulia) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Mahenge akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ghala la kuhifadhi zao la alizeti lililojengwa na Shirika la Farm Africa katika Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka wilayani Ikungi mkoani Singida kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN) kwa gharama ya Sh. 248,324,122 kwa Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA) katika hafla iliyofanyika jana. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Koica Tanzania, Kyucheol Eo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika (AMCOS) Kijiji cha Mnang'ana Yahaya Ramadhani.
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki (kulia) akitoa maelezo ya kilimo chenye tija cha zao la alizeti wakati mgeni rasmi na viongozi mbalimbali walipokuwa wakifanya ukaguzi wa ghala hilo.
Ukaguzi wa ghala hilo ukifanyika.
Ukaguzi wa choo cha ghala hilo ukifanyika.
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa mradi huo.
Wauzaji wa pembejeo za kilimo wakiwa kwenye banda lao wakimsubiri mgeni rasmi kutembelea banda lao.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto akiongoza shughuli mbalimbali za uzinduzi huo.
Mkurugenzi wa Shirika la Farm Africa, Mary Batterman akizungumzia umuhimu wa ghala hilo kwa jamii.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Koica Tanzania, Kyucheol Eo akitoa taarifa kuhusu mradi huo na umuhimu wake kwa wakulima.
Mwenyekiti Msaidizi wa Kampeni ya Kukomesha Vitendo na Matukio ya Ukatili Dhidi ya Jinsia, Wanawake, Watoto na Wazee iitwayo Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida, Ambwene Kajula akiitambulisha kampeni hiyo ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Haika Masawe akitoa taarifa ya ujenzi wa ghala hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIWOHEDE, Justa Mwaituka akichangia jambo kwenye hafla hiyo
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza kwenye hafla hiyo.
Wananchi wa Kijiji cha Mnang;ana wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hafla hiyo ikiendelea.
Wakazi wa Kata ya Sepuka wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Taswira ya uzinduzi huo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki akimkabidhi mgeni rasmi hati ya muongozo wa usimamizi wa ghala hilo.
Hati hizo zikikabidhiwa.
Hati ikikabidhiwa.
Zawadi ya mbuzi ikitolewa kwa mgeni rasmi
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge amewataka wakulima kubadilika na kujipanga na kufanya kilimo biashara na kuachana na kilimo cha mazoea.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu
wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Mulagiri kwa niaba ya Dk. Dk. Mahenge wakati
akizindua ghala la kuhifadhi zao la alizeti lililojengwa na Shirika la Farm
Africa katika Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka wilayani Ikungi mkoani
Singida kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa
Mataifa (UN-WOMEN) kwa gharama ya Sh. 248,324,122 chini ya Ufadhili wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA)
Mulagiri alitaja baadhi ya mambo ya kufanya kilimo biashara ni kuwa na mipango biashara na uzalishaji wa kimkakati, kufahamu kwanza taarifa sahihi za masoko ya alizeti, mahitaji ya soko, wanunuzi, ubora wa mazao, mifumo yao na motisha endelevu za kufanya biashara na wakulima.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kutumia teknolojia zana bora, mbegu bora na pembejeo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, wakulima wajiunge kwenye Ushirika/ vikundi na kuuza kwa pamoja ili kuwa na bei yenye tija, watumie fursa ya kuzungumza na wanunuzi kabla ya kuanza kuzalisha mfano kilimo cha mkataba.idha Mulagiri alisema wafanyabiashara wakubali kuwekeza katika uzalishaji kupitia kilimo cha mkataba baina ya Ushirika/ vikundi vya wakulima na wanunuzi na kuwa zao la Alizeti lina fursa kubwa ya wakulima kupata soko na kujipatia kipato hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa mahitaji ya soko ni zaidi ya mara 3 ya kiasi kinacho zalishwa kwa mwaka.
Mulagiri alitumia nafasi hiyo kuagiza kutumia ghala hilo ambalo pia litatumika kama Kituo cha Huduma za Wakulima kwa kutafakari, na kila mdau kujipanga na Kukuza uelewa wa pamoja kati ya wadau kuhusu mnyororo wa thamani wa zao la alizeti,hususani majukumu kati ya kuzalisha na kuuza kwa tija ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na uratibishaji bora miongoni mwa wadau wa mnyororo wa thamani wa zao la alizeti.
Alisema wakulima wadogo kupitia ushirika na vikundi vyao waunganishwe na masoko makini na yenye tija akitolea mfano Kilimo cha Mkataba na kuachana na mambo ya kuomba omba na kueleza kuwa wanunuzi au taasisi za fedha wawezeshe wakulima kupata pembejeo na fedha za kilimo kupitia mikopo rafiki yenye masharti na riba nafuu inayoendana na hali ya wakulima na kilimo chao kwa ujumla.
"Wakulima wajipange kulima kibiashara na
kuhakikisha kuwa wanayajua vema mahitaji yao, wapi pa kuyapata na kwa muda gani
na kujenga uelewa wao juu ya vichochei na fursa za kilimo endelevu endelevu.
Sio leo msimu mmoja tu umekopeshwa kulima hulimi, kulipa hutaki na unaposhindwa
kutimiza Wajibu wako huji hutoi ushirikiano, hiyo haikubaliki kabisa ni lazima
tufikiri kilimo kama biashara nyingine" alisema Mulagiri.
Mulagiri aliongeza kuwa wataalam wa kilimo waendelee
kuchukua jukumu la Kujenga uwezo wa wadau muhimu katika uwajibikaji wa pamoja
katika uzalishaji, usimamizi wa uzalishaji, ukusanyaji wa mazao, mchakato wa
kuuza kwa pamoja, kusimamia ubora na
mikakati endelevu ya kukuza biashara ya Alizeti.
Aliwataka
wataalam hao wapate uzoefu na tathmini ya mafanikio na changamoto za mnyororo
wa thamani wa zao la Alizeti, kuendeleza mikakati husika kwa ajili ya ufanisi
wa biashara ya Alizeti, kuimarisha ushirikiano na kuwajibika miongoni mwa wadau
na kuwa na mijadala huru ya kibiashara na vishawishi muhimu vya biashara ya
Alizeti na kutambua maeneo muhimu ya kuboresha utekelezaji na ufuatiliaji wa
maendeleo ya uzalishaji na Uuzaji wa ya
Alizeti.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akizungumza kwenye
uzinduzi huo alisema kupata ghala ni
kitu kimoja na kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ni jambo jingine akieleza
kuwa kuna mifano inajionyesha kwani yapo maeneo mengi hapa nchini yamejengwa
maghala lakini sasa yamekuwa ni kumbi za mikutano na disko na ndio maana kwa
Ikungi wamejiongeza kwa kutafuta mfumo uliobora wa matumizi ya ghala hilo
liweze kuwa na tija.
Muro aliomba zitengenezwe kanuni au sheria ndogo
zitakazotumika kuliendesha ghala hilo na kuwa wakati kipindi hiki ambacho Taifa
linapambana na nakisi ya zaidi ya tani 500,000 ya mafuta ya chakula kuagiza nje
ya nchi kwa Mkoa wa Singida ni fursa ya kuashiria alizeti sasa ni Tanzanite na
dhahabu na ni zao lenye thamani kama yalivyo mazao mengine makubwa kama pamba,
korosho na kahawa.
Aliwataka wakulima kutulia na kuacha kufanya kilimo
cha mazoea badala yake walime kilimo chenye tija huku akitolea mfano wakati
wakipata Sh.300,000 kwa kilimo kisicho na tija wenzao wanapata zaidi ya
Sh.Milioni 1 kwa kilimo chenye tija hivyo hatakubali kuona wakulima wakinyonywa
na vishoka kwa kununua gunia la alizeti kwa Sh.30,000 na wao kuliuza kwa
Sh.70,000 wakati hawalimi, hawana mashamb wala hawanunui mbegu labda awe hayupo
katika wlaya hiyo.
“Mwaka huu nimekubali kujitoa kafara ili kumbadilisha
mkulima na usipokubali kubadilika nitakubadilisha kwa nguvu na utabadilika,
tumechoka kila mwaka tunalima pesa haitoshi nataka wakulima wangu wa wilaya ya
Ikungi tulime mjenge nyumba za kisasa, tupate magari na watoto wetu wapate
mitaji na si tulime kwa ajili ya chakula nitazameni tu nimeletwa hapa na Rais
Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuyabadilisha maisha yenu na si vinginevyo”
alisema Muro.
Alisema wataanzisha mfumo wa kuyachukua alizeti kwa
wakulima hao kwa hiyari na hata kwa kutumia nguvu na kwenda kuitunza kwenye
ghala hilo baada ya kufanyika kwa utaratibu maalum wa kuzipokea lengo likiwa ni
kumsaidia mkulima.
Alisema Serikali wilayani humo imejipanga kumsaidia
mkulima ambaye atakuwa na subira ili alizeti anayoilima iwe msaada wa kubadili
maisha yake ambapo alitumia kuwaomba wakina mama kuwahimiza waume zao kupeleka
alizeti kuhifadhiwa katika ghala na kuja kuiuza kati ya Sh.80,000 hadi 100,000
badala ya Sh.30,000 na Sh.40,000.
Akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa UN-WOMEN
Tanzania, Mratibu wa Mradi wa Tuufikie Usawa wa Jinsia kupitia kuwawezesha
Wanawake na Wasichana, Lilian Mwamdanga alisema mradi huo
unatekelezwa na UN-WOMEN kwa kushirikiana na UNFPA kupitia ufadhili wa Koica na
kuwa UN- Women imekuwa ikiongoza kipengele cha kuwezesha wanawake kiuchumi
hususan kuwajengea uwezo wanawake wakulima wadogowadogo katika mazao ya mboga
mboga na alizeti katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kuwa uzinduzi wa
ghala hilo ni sehemu ya mradi huo.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili mradi huo
umewafikia wakulima zaidi ya 1000 ambao ni wa mboga mboga na alizeti kutoka
katika Kata za Sepuka, Irisya na Dung'unyi na kati yao wanawake ni asilimia 80.
Akitoa taarifa ya utekeleza wa mradi huo kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Afisa Maendeleo ya Jamii wa
wilaya hiyo, Haika Masawe alisema lengo la mradi huo ni kuwawezesha
wakulima kuongeza thamani ya zao la alizeti kwa kutunza mazao yao kwa pamoja
wakisubiri bei yenye tija ili kuwawesha wanachama/wakulima kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.
Masawe alisema ujenzi wa
ghala hilo ulianza Mwezi Novemba mwaka 2021 na kukamilika mwezi wa Machi mwaka
2022 chini ya mkandarasi Manyara Contractors akisimamiwa na Mhandisi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na Mkuu wa Idara ya Kilimo,Umwagiliaji na
Ushirika.
Alisema Ghala hilo lina uwezo wa kuhifahdi zaidi ya kilo la 300,000 sawa na gunia 5000 za alizeti (sawa na tani 300) na kuwa lina vyumba vitatu ambapo kimoja ni ofisi ya chama cha ushirika Mnang’ana, Stoo ya kutunzia pembejeo ambayo pia inaweza kutumika kama duka la pembejeo za kilimo, ukumbi mdogo wa mikutano na mafunzo ya chama cha ushirika na kuwa ujenzi wa ghala hilo umegharimu jumla ya Sh.248,324.122.
Post A Comment: