Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Singa Kata ya Kinampundu katika ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) aliyoifanya hivi karibuni wilayani Mkalama.
Wananchi wakijiji cha Singa wakicheza ngoma wakati wakimkaribisha Mkuu wa wilaya katika ziara hiyo.
Wananchi wa kijiji cha Singa wakiwa kwenye mkutano wa mkuu wa mkoa .
Katibu tawala wa Wilaya ya Mkalama,.Elizabeth Rwegasira akifanya utambulisha kwa watumishi wa Halmashauri pamoja na msafara uliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Diwani wa Kata ya Mwangeza ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Mkalama, Bosco Samwel akizungumza kwenye ziara hiyo.
Wananchi wa Kijiji cha Munguli Kitongoji cha Kipamba wakitumbuiza kwa ngoma za asili za jamii ya Wahadzabe wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Kijiji cha Munguli.
Afisa Mazingira Wilaya ya Mkalama, Amon Sanga akieleza utekelezaji wa mradi wakurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula unaotekelezwa katika Kata ya Mpambala kwa vijiji vya Nyahaa, Mkiko, Mpambala , Lugongo pamoja na Kata ya Mwangeza Kijiji cha Munguli.
Mratibu wa Sensa Wilaya ya Mkalama, Daniel Tesha akieleza maandalizi ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.
Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe Edward Mashimba akitoa neno la shukrani kwa ujio wa Mkuu wa Mkoa katika Kitongoji cha Kipamba ambapo alisema jamii ya Wahadzabe iko tayari kushiki shughuli zote zamaendeleo pamoja na kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi ifikapo Agost 23 mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Mahenge akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa jamii ya wahadzabe pamoja na wataalamu mbalimbali wakati wa ziara hiyo.
Rachel Joram na Dotto Mwaibale, Mkalama
MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt . Binilith mahenge ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutenga kiasi cha sh.2,118,079,899.00 kutoka kwenye mfuko wa kimataifa wa mazingira katika kutekeleza mradi wa kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika kata ya Mpambala na Kata ya Mwangeza Kijiji cha Munguli Wilaya ya Mkalama mkoani Singida
Dkt. Mahenge aliyasema hayo katika ziara aliyoifanya wilayani hapa ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo wa kunusuru Kaya Masikini (TASAF) katika Kijiji cha Singa Kata ya Kinampundu na Kijiji cha Munguli Kitongoji cha Kipamba Kata ya Mwangeza na kusema kukamilika kwa mradi hiyo itatatua changamoto nyingi za wananchi ikiwani pamoja na kutatua kero za maji, na kutunza mazingira , kuzuia mmomonyoko kwenye maeneo yanayotekelezwa miradi.
Aidha amewataka wataalamu wa ngazi zote kusimamia vizuri pamoja kushirikiana kutatua changamoto zitakazojitokeza ili kuharakisha maendeleo ya Wananchi wa wilaya ya mkalama ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro mbalimbali iliyopo katika maeneo ya miradi.
Akitembelea bwawa la kijiji cha Singa kata ya Kinampundu liliochimbwa na wanufaika wa mradi wa kunusuru kaya masikini TASAF aliwataka wananchi hao kutumia mradi huo vizuri ili uweze kuwanufaisha kwakuwataka kulima kilimo cha umwagiliaji na kutoruhusu mifugo kuingia na kukanyaga kujaza mchanga kwenye mradi ili maji hayo yaweze kudumu hadi kipindi cha masika.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo alianza kwa kumshukuru Mkuu wa Mkoa kutembelea wilaya ya mkalama kujionea maendeleo ya wilaya na kuongeza kuwa ziara yake inachochea kasi ya maendeleo kwani wananchi wanajisikia furaha kutembelewa na viongozi wa kubwa huku akimuomba Mkuu wa mkoa Dkt . Mahenge inapotokea kugawanywa maeneo ya utawala na Kata ya Mwangeza iangaliwe kwa jicho la pekee kwani ni kubwa hivyo kupunguza ufanisi wa kuwafikia wananchi waliopo maeneo ya mbali.
Diwani wa Kata ya Mwangeza Bosco Samwel aliongeza kuwa ni kweli Serikali imefanya mambo makubwa katika kata yake na hasa kwa jamii ya Wahadzabe inayoishi kijiji cha Munguli kitongoji cha Kipamba lakini kilio bado kipo kwenye ubovu wa miundo mbinu ya barabara , umeme, ukosefu wa nyumba za walimu pamoja na uhaba wawalimu katika shule shikizi ya Kipamba ambayo tayari imesajiliwa pamoja na shule shikizi ya Mwasulagi ambayo hakuna barabara ya kufika katika shule hiyo.
Afisa Mazingira Wilaya ya Mkalama Amon Sanga alieleza utekelezaji wa mradi wa mazingira umesaidia kuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji vitano vinavyotekeleza mradi wa LDFS ,huku vikundi vya uzalishaji kiuchumi vikianza kunufaika na ufugaji kwa kupata mizinga ya nyuki 420 pamoja na kuwepo kwa msitu ambao tayari una hati miliki ya kimila unaotoa manufaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufugaji wa nyuki, upatikanaji wa mahitaji ya jamii ya kihadzabe kama vile dawa,mizizi , matunda na wanyama pori.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa TASAF Mratibu wa TASAF Wilaya ya Mkalma, Gudluck Mlau alisema kuwa kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Mei 2022 Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama im epokea kiasi cha Tsh,.1,591,881,600.00 na malipo yamefanyika katika vijiji vyote 70 ambapo jumla ya walengwa 7,235 walinufaika na mradi huo huku kijiji cha Munguli kikipokea fedha za ruzuku kiasi cha Tsh.43,998,000.00 kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Mei 2022 huku walengwa 354 wakipokea ruzuku zao kwa njia ya mtandao jambo linalowapa urahisi wakupokea fedha zao .
Sanjari na hayo Mratibu wa Sensa Wilaya ya Mkalama, Daniel Tesha alieleza maandalizi ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu kuwa yanaendelea vizuri na kuongeza kuwa tayari hamasa imeshafanyika kwa vijiji vyote70 vya wilaya ya Mkalama na tayari eneo Maalumu limetengwa katika kitongoji cha Kipamba kijiji cha Munguli maalumu kwa jamii ya wahadzabe na bajeti maalumu imewasilishwa ofisi ya Takwimu taifa ili jamii hiyo iweze kupata chakula katika siku hiyo ya sensa na kuweza kushiriki kikamilifu.
Baadhi ya wananchi wajamii ya wahadzabe wameishukuru serikali kuweka kipaumbele na kupeleka miradi mingi katika jamii hiyo huku wakiaahidi kuunga mkono juhudi za serikali kwa kufanya kazi kwa bidii na kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi ifikapo Agosti 23 mwaka huu.
Post A Comment: