Na John Walter-Manyara

Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa kushirikiana na jeshi la polisi mkoani Manyara limeanza operesheni ya kuwabaini wezi wa miundombinu ya umeme ambapo Watu saba wamekamatwa katika wilaya ya Babati.

Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Manyara Mosses Kisanza amesema walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba katika kijiji cha Shaurimoyo waya katika nguzo 13 zimekatwa na watu wasiojulikana.

Aidha waligundua mradi uliojengwa kinyume na taratibu za shirika hilo (ILLEGAL) katika kijiji cha Kiru Six wilayani Babati ambapo zimejengwa nguzo tano na kuunganisha waya zikisubiri kuwaunganishia wateja.

Kisanza amesema katika operesheni hiyo walibaini uharibifu kufanywa katika nguzo kubwa (Gridi ya taifa) 220KV kutoka kituo cha kupooza Umeme cha wilaya ya Babati kwenda Arusha ambapo kuna baadhi ya vyuma vimefunguliwa kwenye nguzo zilizopo katikati ya Minjingu na Mbuyu wa Mjerumani.

Katika hatua nyingine Kisanza amewaomba wananchi na wasamaria wema kushiriki katika kutoa taarifa za siri ambazo zitafanikisha kuwakamata wananchi wanao hujumu miundmbinu ya umeme.

Hata hivyo shirika la Umeme mkoani Manyara bado linafanya tathmini juu ya uharibu uliofanywa. 

Akizungumzia tukio la watuhumiwa hao saba wa miundo mbinu ya TANESCO Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara Benjamin Kuzaga amesema watu hao watafikishwa mahakamani muda wowote upelelezi ukikamilika.

Amesema kwa kushirikiana na TANESCO walifanya msako maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara ambapo walifanikiwa kukamata baadhi ya vyuma ambavyo vinatumika kwenye miundombinu ya TANESCO kwenye nguzo zake za chuma.




Amesema walivikuta vyuma hivyo katika gereji mbalimbali na vingine katika makazi ya watu.


Share To:

Post A Comment: