Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amepongeza bunifu mbalimbali zinazojikita katika kutatua changamoto za kimsingi zinazoikabili jamii na kutaka wabunifu hao walelewe na kuendelezwa ili kutoa mchango katika maendeleo ya nchi kwa kuchochea uchumi na kuboresha huduma za kijamii.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo wakati alipotembelea Maonesho ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ya mwaka 2022.
“Vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi vinapaswa kutumia fursa ya maonesho haya kujitathmini na kujipima ili kuona ni kwa namna gani vinaweza kutoa Elimu na Mafunzo ya Ufundi bora yatakayotatua changamoto za kiuchumi na kijamii hapa nchini sambamba na kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira na kutoa fursa kwa vijana kujiajiri.
Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 imeweka wazi kuwa elimu ni kipaumbele cha juu kwani ndiyo kitovu cha kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwenye jamii.
Mafunzo ya ufundi na ufundi stadi hujulikana kwa mchango wake mkubwa katika ukuaji wa maendeleo ya viwanda, uchumi na ustawi wa jamii katika nchi yoyote.Hivyo ni vyema kuendelea kuweka msisitizo katika mafunzo haya kwa mustakabali wa maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu.
Nimefurahi kuona vijana wengi wa kitanzania wakija na ubunifu mzuri ambao unalenga kuboresha huduma za jamii na kukuza uchumi,vijana hawa wanapaswa kuendelezwa ili kuja kutoa mchango wao mkubwa katika ujenzi wa Taifa Tanzania”Alisema Mavunde
Katika ziari hiyo fupi Mh Mavunde aliongozana na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uongozi NACTE Prof. John Kondoro na Katibu Mtendaji wa NACTE Dr.Adolf Rutayuga
Post A Comment: