Na John Walter-BabatiMkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amekabidhi Pikipiki sabini moja (71) kwa Maafisa Ugani waliopo katika Halmashauri mbili za wilaya hiyo kwa lengo la kuwarahisishia kazi ya kuwahudumia wafugaji katika maeneo yao.
Akikabidhi pikipiki hizo, Twange amesema ugawaji wa pikipiki hizo kwa maafisa hao ni katika jitihada za serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha sekta hiyo ili iweze kuwa na tija kubwa kwa Taifa.
Amesema kutokana na changamoto ya Wakulima kutotembelewa kwa wakati, wamekuwa hawapati huduma yenye tija kwa kutembelewa mara chache na wataalamu, na hivyo kuwa na uzalishaji hafifu.
Maafisa Ugani katika Halmashauri ya wilaya ya Babati wamekabidhiwa pikipiki 50 na Babati mji pikipiki 21 na kufanya jumla kuwa 71.
Twange amesema, wananchi bado wanalima kilimo cha mazoea kutokana na kukosa wataalamu wa kuwapa elimu hivyo upatikanaji wa pikipiki hizo utasaidia kukuza uchumi kupitia kilimo kwa Wakulima kupata elimu na ushauri.
"Pikipiki hizi zitawasaidia Maafisa Ugani kuwatembelea Wakulima kwa wakati na kuwapa huduma ambazo zitawawezeaha kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo, " alisema Twange.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Babati Anna Fissoo amesema pikipiki hizo zitakwenda kuondoa changamoto katika shughuli za ugani katika Halmashauri hiyo kwani zitawawezesha kuwafikia Wakulima ambao wapo katika Vijiji na Vitongoji.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Babati Abdulrahmani Kololi amesema watasimamia pikipiki hizo huku akitoa wito kwa maafisa ugani waliokabidhiwa kuhakikisha wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, na kuepuka kuzitumia kama za biashara kwa kubeba abiria na kufanyia shughuli binafsi.
Mmoja wa maafisa Ugani kutoka kata ya Singe Eveta Lyatuu aliishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kuwapatia usafiri ambao utawarahisishia utendaji.
Serikali imetumia Shilingi Milioni 864 kununua pikipiki hizo ambazo zinasambazwa kwenye mikoa 25 na Halmashauri 140 zitafaidika na pikipiki hizo.
Post A Comment: