Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk.Angeline Mabula akizungumza katika hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama ,Sophia Kizigo akizungumza wakati wa zoezi la utoaji hatimiliki hizo.Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk.Angeline Mabula na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo (kushoto) wakiserebuka na Wanawake wa Kikundi cha Sanaa cha Jamii ya Wawindaji ya Wahadzabe wa Kijiji cha Munguli Kata ya Mwangeza wilayani Mkalama.
Watoto wakiwa kwenye hafla hiyo.
Diwani wa Kata ya Mwangeza Bosco Samwel akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mkalama, Lameck Itungi akizungumza kwenye hafla hiyo.
Wanawake wa Jamii ya Wahadzabe wakimpa heshima ya kumvika shanga za kimila Dk. Angeline Mabula katika hafla hiyo.
Wanawake wa Jamii ya Wahadzabe wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wananchi wa Jamii ya Wahadzabe wakisubiri kupatiwa hati zao.
Hati zikikabidhiwa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo (kulia kwake) na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Jamii ya Wawindaji ya Wahdazabe baada ya kuwakabidhi Hatimiliki za kimila za kumiliki ardhi ambapo hati 100 walikabidhiwa.
Chifu wa Jamii ya Wawindaji ya Wahadzabe Edward Mkumbo akifurahi na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Shamim Hoza baada ya kukabidhiwa hatimiliki yake.
Wasanii wa kikundi cha Utamaduni cha Jamii ya Wahadzabe wakiwa wamejipanga kwa ajili ya kutoa zawadi kwa Dk. Mabula na viongozi wengine meza kuu.
Dk. Mabula akipokea zawadi ya asali.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza baada ya kupata maelezo ya ujenzi wa jengo la makumbusho la Jamii ya Wawindaji ya Wahadzabe kutoka kwa Diwani wa Kata ya Mwangeza, Bosco Samweli (kulia) ambapo aliahidi kuchangia mifuko hamsini ya saruji.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalamam Elizabeth Rwegasi akitoka kwenye nyumba ya Chifu wa jamii hiyo wakati wa ziara ya utoaji hatimiliki za kimila
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula akitoka kwenye nyumba ya Chifu wa jamii hiyo wakati wa ziara ya utoaji hatimiliki za kimila. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo.
Sara Abel kutoka Jamii ya Wahadzabe akimpatia maji mtoto wake Kizali George wakati wa hafla hiyo.Sara ni mmoja wa jamii hiyo waliopata hatimiliki ya ardhi ambayo ndio urithi wa baadaye wa mtoto huyo baada ya masomo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
JAMII ya Wawindaji ya Wahadzabe
iliyopo Wilaya ya Mkalama mkoani Singida imeipongeza Serikali kwa hatua
iliyoichukua ya kuwapimia maeneo yao na kupatiwa hatimiliki za kimila na kuwa
sasa wataacha maisha ya kuhamahama na kujikita katika shughuli za maendeleo.
Kupata kwa hatimiliki hizo kunafungua milango ya fursa kwa jamii hiyo
inayojishughulisha na uwindaji huku chakula chao kikiwa ni matunda pori, asali
na uchimbaji wa mizizi ambayo waitumia kama chakula na dawa kwa ajili ya kujitibu.
Hatua hiyo ya kuwapimia ardhi na kuwapatia hatimiliki inamfanya kila
Muhadzabe kumiliki ardhi yake hivyo kuepusha kabisa na uwezekano wa kugombea
maeneo ya uwindaji na shughuli zingine zinazohitaji matumizi ya ardhi.
Akizungumza jana katika hafla ya kukabidhiwa hati 100 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Angeline Mabula kwa niaba ya
wenzake Mwenyekiti wa jamii hiyo, Edward Mkumbo alisema sasa wameacha kabisa
kuhamahama kama ilivyokuwa awali na kuwa
wameanza kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo tofauti na zamani.
"Tunaishukuru Serikali ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea jambo ili zuri na kuitambua
jamii yetu na kutupimia ardhi yetu itatusaidia kwani tayari tulisha anza
kuvamiwa na wafugaji kutoka mikoa mingine na kutushia mustakbari mzima wa
maisha yetu" alisema Mkumbo.
Akizungumza na jamii hiyo ya wawindaji ya Wahadzabe katika Kijiji cha
Munguli, Kitongoji cha Kipamba Kata ya Mwangeza wilaya humo Dk.Mabula alisema,
jamii hiyo ni miongoni mwa jamii ndogo nchini ambayo iko katika hali ya
kupoteza ardhi wanayoimiliki kutokana na jamii nyingine kuingia na kufanya
shughuli zisizoendana na tamaduni za jamii hiyo jambo alilolieleza
linahatarisha ustawi na maisha na desturi za Wahadzabe na kuwa Serikali
haitakuwa tayari kuona jambo hilo likitokea.
‘’Serikali haitakubali kuona ardhi
inayotumiwa na jamii hiyo ikipotea kwani katika miaka ya hivi karibuni jamii ya
Wahdzabe imekuwa ikikabiliwa na tishio
la kutoweka na kupoteza uhalisia wa maisha yao baada ya baadhi ya wananchi kutoka
maeneo mengine kuingia katika maeneo ya mapori ya asili wanayoyatumia na kuanza
kuyavamia kwa ajili ya shughuli za ufugaji, kilimo na upasuaji wa mbaoi’’ alisema Dk. Mabula
Alitaja baadhi ya matishio ya maeneo hayo ni kuanza kupotea kwa makazi ya asili yanayojengwa kwa nyasi
kavu chini ya matawi ya miti, wanyama kutoweka, mizizi na matunda kupotea
kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli nyingine ambazo hazilindi uoto
wa asiili wa mapori hayo.
Dk.Mabula alisema kwa kutambua
athari inayoweza kujitokeza dhidi ya jamii hiyo Serikali kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali wanatafuta njia bora ya
kulinda jamii hiyo na wananchi wengine ili kuhakikisha kuna kuwa na usawa kwa
wote katika matumizi ya rasilimali za ardhi hapa nchini.
Aidha Dk.Mabula alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dk.Binilith Mahenge na watendaji wote wa idara ya ardhi mkoani hapa na wilaya
ya Mkalama hasa Kamishna wa Ardhi Msaidizi i Mkoa wa Singida Shamim Hoza kwa
kufanikisha mpango huo.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo alisema, jamii ya Wahadzabe katika
eneo hilo la Kijiji cha Munguli Kata ya Mwangeza na baadhi ya maeneo
kumekuwa na changamoto ya migogoro ya
ardhi hasa inayohusu mipaka.
‘’Changamoto yetu kubwa hapa, jamii ya Wahadzabe vyakula wanatoa porini,
wanakula asali na nyama za kuwinda na misitu ikiharibiwa au maeneo
wanayotegemea kupata vyakula yanapoharibiwa ni changamoto kubwa, hata hivyo
nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa uvumilivu wao wa muda mrefu’’ alisema Kizigo.
Katika hafla hiyo baadhi ya wananchi wa eneo hilo walipata fursa ya kuzungumzia changamoto mbalimbali za migogoro ya ardhi akiwemo Diwani wa Kata ya Mwengeza Bosco Samweli, ambaye alimueleza Dk Mabula kuwa, eneo hilo la jamii ya Wahadzabe kwa muda mrefu limekuwa na changamoto ya migogoro ya mpaka na wananchi wanaoishi wilaya za jirani za Karatu Arusha na Mbulu mkoa wa Manyara na kuwa sasa zinaelekea kumalizika kutokana na juhudi kubwa inayofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo ya kuzitatua akishirikiana na maafisa ardhi wa wilaya hiyo na wataalam wengine.
Post A Comment: