Diwani wa Kata ya Mwaru Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Iddi Athumani Makangale (katikati) ambaye ni muumini wa dini ya Kiislam akiongoza harambee ya ununuzi wa vyombo vya muziki vya Kanisa la Waadiventista Wasabato la Kijiji cha Kaugeri katika changizo lililofanyika hivi karibuni ambapo zaidi ya Sh. Milioni 1.7 zilipatikana. Kushoto anayechangia katika harambe hiyo ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Kaugeri, Ukunde Mshele.

Mchungaji, Paul Kilo akitoa Shukurani kwa Mgeni rasmi wa harambee hiyo Diwani wa Kata ya Mwaru, Iddi Makangale baada ya kuongoza  harambee hiyo. Kutoka kushoto ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Geofyey Mgonja na Afisa Mtendaji wa Kata ya Kaugeri, Ukunde Mshele. 

Diwani Makangale akiwa na viongozi mbalimbali wakati wa changizo hilo.

Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo,  Geofrey Mgonja akizungumza wakati akimshukuru Diwani Makangale kwa   kuongoza harambee hiyo. Katikati aliyefunga skafu ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kaugeri, Hassan Omari.

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

DIWANI wa Kata ya Mwaru katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Iddi Athumani Makangale ambaye ni muumini wa dini ya Kiislam ameongoza harambee ya ununuzi wa vyombo vya muziki vya Kanisa la Waadiventista Wasabato la Kijiji cha Kaugeri ambapo zaidi ya Sh. Milioni 1.7 zilipatikana.

Akizungumza katika changizo hilo Makangale alisema amejisikia furaha ya kualikwa kuongoza harambee hiyo hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni Muislam jambo ambalo limezidi kuongeza mshikamano baina ya Waislam na Wakristo.

" Tukio ili limenipa furaha sana n.a. linaonesha ni jinsi gani waumini wa hizi dini mbili wanavyoshirikiana katika shughuli zao" alisema Makangale.

Alisema katika harambee hiyo iliyoonesha mafanikio makubwa jumla ya Sh. 1,785,000 zilipatikana huku ahadi zikiwa ni Sh.470,000.

Diwani Makangale alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi wa dini hizo na waumini wao kuendelea kudumisha ushiriano huo katika shughuli mbalimbali jambo litakalosaidia kuharakisha maendeleo katika kata hiyo.

Akizungumza baada ya harambee hiyo  Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo Geofrey Mgonja alisema wamefarijika sana kwa harambee hiyo iliyoongozwa na diwani huyo na kueleza ni jambo la kuigwa kwa waumini wote wa dini hizo.

Alisema tukio la namna hiyo liliwahi kufanywa na Aliyekuwa Rais wa Tano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli pale alipoongoza harambee ya ujenzi wa Msikiti wa Chamwino mkoani Dodoma.

"Tuna kila sababu ya kukushuku Mheshimiwa diwani kwa jambo ili kubwa ulilolifanya la kutuongozea harambee hii Mungu akubariki sana na kukupa afya na maisha marefu pia abariki na utumishi wako wa kuwatumikia wananchi bila ya kubagua dini zao" alisema, Mgonja.

Aidha Mchungaji Mgonja alitumia nafasi hiyo kwanza kabisa kumuomba Rais Samia Suluhu Hassan, Makanisa ya Wasabato, Waislamu kote nchini, viongozi na wadau mbalimbali waliopo ndani na nje ya Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida na Wananchi kwa ujumla kuwasaidia ili waweze kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha hitaji lao la Sh. Milioni 10 kwa ajili ya kupata vyombo hivyo vya muziki vitakavyo saidia kuhubiri neno la Mungu kwa njia ya uimbaji na kuwa atakaye kuwa tayari kutoa kiasi chochote alichonacho bila ya kuhesabu kuwa ni kidogo kwao kitakuwa kikubwa hivyo anaweza kuwasiliana naye kwa namba 0733445310 au kutuma fedha hiyo kupitia namba ya M-PESA-0766978916 au kuwasiliana na Mwandishi wa habari wa taarifa hii kwa namba ya simu 0754362990  na Mungu atambariki kwani kutoa ni moyo wa mtu na si fedha.


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: