Na Mwandishi Wetu.
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu leo imeingia makubaliano ya kuwanoa wanagenzi 75 katika fani za ufundi bomba na mafundi umeme wa majumbani.
Makubaliano hayo yamesainiwa jijini Dodoma kati ya Mkuu wa Taasisi hiyo Profesa Preksedis Ndomba na Festo Fute kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wakikabidhiana makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Kijoli Saidi amesema huo ni muendelezo wa mafunzo hayo ambayo ni endelevu ambapo ofisi ya Waziri Mkuu imekua ikisaidia vijana kupata mafunzo ikiwa ni sehemu ya kutengeneza ajira kwa vijana.
"Katika kutengeneza ajira, Idara ya Ajira na Ukuzaji Ujuzi inatoa mafunzo mbalimbali ikiwa ni kwa lengo la kurasimisha ujuzi kwa vijana nje ya mfumo rasmi," amesema Kijoli.
Aidha, amesema lengo jingine la mafunzo hayo ni kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana waliokosa kuendelea na masomo katika fani mbalimbali ili waweze kujiajiri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa DIT Kampasi ya Myunga, Dkt. Frank Lujaji amesema kati ya vijana hao 75, wakike ni 33, na kwamba mafunzo ni ya miezi sita darasani na miezi miwili wakifanya mafunzo viwandani.
"Awamu ya kwanza ya mafunzo haya tulikua pia na vijana 75 ambao baada ya kuhitimu zaidi ya asilimia 50 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali na hawa walikua ni mafundi bomba na wataalam wa TEHAMA," amesema Dkt Lujaji.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Prof Preksedis Ndomba ameishukuru ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuitumia DIT kuwasaidia vijana katika Mkoa wa Songwe ambao una uhitaji wa wataalam mbalimbali.
Post A Comment: