Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza kwenye hafla hiyo. |
Mwakilishi wa Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN), ambaye pia ni Mtaalam wa Kitengo cha kuwawezesha wanawake kiuchumi, Lilian Mwamdanga akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro amewataka wakulima wilayani humo
kuhifadhi mazao ili waje kuyauza kwa bei yenye tija.
Muro alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akiweka jiwe la Msingi la Mradi wa Ghala la zao la alizeti ambalo limejengwa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya
Sepuka na Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN) kwa Sh. 248,324,122 kwa Ufadhili wa Shirika la
Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Japani (KOICA) mradi ambao unatekelezwa na Shirika la Farm Africa chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
“ Nataka mwaka huu wakulima wote wa zao la alizeti wanufaike kwa kuuza kwa
bei nzuri na kuacha kurubuniwa na walanguzi (vishoka) ambao wamekuwa
wakiyanunua kwa bei ya chini na kwenda kuyauza kwa bei ya juu" alisema
Muro.
Muro aliishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa
kuwapelekea mradi huo ambapo pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wa
maendeleo Konica , UN-WOMEN na Farm Africa kwa kutekeleza mradi huo wa ujenzi wa
ghala hilo.
Muro aliwataka wazazi kuwapeleka watoto wao shule za ufundi VETA ili baada ya masomo waweze kupata
mkopo wa asilimia 10 unaotolewa na
halmashauri waweze kukopa mashine za kuchomelea, kununua vyerehani na kufungua
viwanda vidogo kama vya ushonaji wa nguo, utengenezaji wa vifaa vya chuma (welding) badala ya kuwaacha waende mjini hasa wasichana kutafuta kazi za ndani.
Alisema Serikali imepanga kila
kijiji hapa nchini kuhakikisha kinapata umeme na kuwa kwa Wilaya ya Ikungi
wanataka umeme huo ufikishwe kwenye maeneo ya kimkakati akitolea mfano Kata ya
Iyumbu ambayo ni maarufu kwa kilimo cha mpunga ambapo badala ya kuuza mpunga
waanze kuukoboa na kuuza mchele ambao mifuko yake itawekwa lebo ya Ikungi
jambo litakaloongeza thamani ya zao hilo na Serikali kupata mapato.
Muro alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki
zoezi ya Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23 miaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi aliwashukuru wadau hao kwa hatua walioifikia ya kujenga Ghala hilo la kisasa na kuwashukuru wananchi wa Kata ya Sepuka na Kijiji cha Mnang'ana kwa kukubali kutoa eneo la ujenzi.
Alisema ujenzi wa ghala hilo ulianza mwezi Novemba mwaka jana na kukamilika
Machi mwaka huu na kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza thamani ya zao la
alizeti kwa wakulima kwa umoja wao waweze kuyahifadhi wakati wakisubiri bei yenye tija na kuwawezesha
kujipatia kipato cha kujikimu kiuchumi.
Alisema mradi huo ni matokeo ya shughuli zilizotakiwa kutekelezwa kupitia Mradi wa Tuufikie Usawa wa Kijinsia kwa kumuwezesha Mwanamke na Msichana na kutambua
mahitaji ya kijamii.
Kijazi alisema katika ghala hilo
vimewekwa vifaa mbalimbali kama mzani wa kidigitali, kipima unyevu, projekta,
mashine ya kudurufu na kutoa nakala,machekeche, mitungi ya kuzimia moto na
samani za aina mbalimbali na kuwa lina uwezo wa kuhifadhi tani 300 au kilo 5000 za zao la alizeti.
Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa wilaya hiyo, Gurisha Msemo alisema wamejipinga vilivyo
kuhakikisha vipimo vitakavyotumiwa kuuza mazao ya wakulima ni vile
vilivyopendekezwa na Serikali na si vinginevyo ili wakulima waweze kunufaika na
kilimo.
Post A Comment: