Na Mwandishi Wetu, Kakonko
CHAMA cha Ushirika cha Muungano Kiziguzigu Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma
kinatarajia kuuza tani 400 za zao la maharage kwa Shirika la Mpango wa Chakula
Duniani (WFP) na wanunuzi wengine katika msimu huu wa 2021/2022.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Ushirika huo, Jackson Bujege wakati
akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea chama hicho na kuona
shughuli ambazo wanafanya.
Bujege alisema wakulima wa maharage wameongeza uzalishaji baada ya kupata
Mradi wa Kigoma Pamoja Program (KJP), ambapo kwa upande wa kilimo unatekelezwa na WFP, Kituo cha Biashara cha
Kimataifa (ITC), Shirika la Uendelezaji wa Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF)
na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).
Alisema mashirika hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji,
ubora wa mazao na masoko hivyo watahakikisha manufaa hayo yanaendelea.
“WFP wamekuja kutukomboa ambapo baada ya mradi kuanza mwaka 2018 walinunua
tani 100 za maharage, msimu wa pili tani 368 na msimu huu tunatarajia kuuza
tani 400 kwa sh.1950 hadi 2,000,” alisema.
Bujege alisema katika misimu hiyo miwili wakulima ambao ni wanachama wa
AMCOS waliweza kuingiza sh.milioni 717, fedha ambazo zimetumika kuchochea
shughuli za maendeleo na kilimo.
“AMCOS hii ina wanachama 308 ambapo wanaume ni 200 na wanawake 108, ila
tunaendelea kuhamasisha wanachama wanawake kujiunga ili kuweza kuwainua,”
alisema.
Alisema mikakati ya chama chao ni kuhakikisha uzalishaji unaongezeka hadi
kufikia tani 1,000 za maharage.
Ofisa Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Kakonko, Khalfan Muhidin
alisema halmashauri hiyo inafurahi ujio wa WFP na mashirika mengine ambapo
zaidi ya wakulima 1,800 wamepata elimu kuhusu uhifadhi mazao, mbinu za kulima,
kupunguza upotevu wa mazao yakiwa shambani na masoko.
“Wananchi wengi wamehamasishwa kukusanya mazao katika eneo moja, kwani bei
yake ni kubwa na wakulima wananufaika,” alisema.
Ofisa huyo alisema ujio wa mradi huo umeongeza mapato kwa halmashauri
ambapo mwaka jana wamekusanya ushuru zaidi ya Sh.milioni 21.8 kutoka Sh.milioni
tano zilizokuwa zikakusanywa awali.
Alisema wataendelea kutoa elimu kwa wakulima zaidi ya 200,000 walioko
kwenye wilaya hiyo, ili kuhakikisha wanaongeza uzalishaji na kujiunga na vyama
vya ushirika.
“Lengo ni kuongeza uzalishaji kupitia AMCOS zilizopo ambapo kwa sasa tuna
Gwarama, Muungano, Kabingo, Kuchikeka na Kanyonza,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Mallasa alisema ujio wa mashirika
hayo wilayani kwake umechangia shughuli za uchumi na maendeleo kukua kwa kasi.
Naye Mkuu wa Ofisi ya WFP Kibondo, Saidi Johari alisema katika msimu huu
wanatarajia kununua tani 3,000 za maharage kutoka kwa wakulima mbalimbali
nchini.
Post A Comment: