Mwalimu wa Ujasiriamali ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Itigi Mjini
Saimon Sirilo akitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana wa Kata hiyo yaliyofanyika wilayani humo mkoani Singida jana. 


Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Paschal Masele akitoa mafunzo kwa vijana hao.

Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Paschal Masele (kulia) akiteta jambo na mratibu wa mafunzo hayo, Saimon Sirilo wakati wa mafunzo hayo.
Igizo la watoa huduma wanao wajali wateja wao na wale wasio wajali likifanyika.

 Vijana wa Kata ya Itigi Mjini wakiwa katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wao Saimon Sirilo (waliokaa kushoto na Paschal Masele kulia) baada ya kupata mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika wilayani humo mkoani Singida jana.



Na Dotto Mwaibale, Itigi


VIJANA zaidi ya 30 wa Kata ya  Itigi mjini katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili yaweze kuwasaidia kuwainua kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mratibu wa mafunzo hayo Mwalimu wa ujasiriamali Saimon Sirilo ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Kata hiyo alisema mafunzo hayo yametolewa bure ili kuwasaidia vijana wa Kata hiyo kujikwamua kiuchumi.

"Lengo la kutoa mafunzo haya ni kuwafanya vijana wajiweke katika mazingira mazuri ya kiuchumi na sio tu kulia ukosefu wa ajira huku sisi watendaji tukiwapitishia barua na kugonga mihuri pasipo kuwajengea uwezo wa kujikomboa kiuchumi na kutimiza dhana nzima ya kuwatumikia wananchi" alisema Sirilo.

Alisema mafunzo hayo yatakuwa endelevu lengo likiwa kuwafungulia dunia vijana wa Itigi ili waweze kuyaona mengi mazuri yenye faida yaliopo katika tathinia ya ujasiriamali.

Alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo vijana hao wa ufahamu chanya kuhusu masuala ya fedha, bajeti, huduma kwa wateja, dhana ya ujumla ya ujasiriamali na namna ya kuzitambua fursa zilizopo Itigi.

Alisema baada ya kupata mafunzo hayo vijana hao walifanya igizo kuonesha baadhi ya watoa huduma wasiowajali wateja wao hivyo kusababisha wawakimbie na wale wanaowajali wateja ambapo walionekana kuzikuza biashara zao huku dhana nzima ya mteja ni mfalme ikijidhihirisha.

Aidha Sirilo aliwakumbusha vijana hao  juu ya ufahamu chanya kuhusu mambo ya fedha na kuwaeleza wanapaswa kujiuliza kuwa pesa zao huwa zinakwenda wapi kwa kuwa kila siku wanazipata lakini hakuna wanachokifanya zaidi ya kuendelea kulalamika kuwa maisha ni magumu.

Alisema vijana wengi matumizi yao ya fedha sio sahihi kwani huzitumia vibaya na kusahau kufanya vitu vya msingi na ili wafanikiwe wanapaswa kuwekeza zaidi na kuwa na vipaumbele, kufanya mambo ya lazima na sio ya muhimu.

Pia aliwakumbusha kuwa fedha zimejificha katika mazingira kadhaa kama vile katika mikono ya watu, kwenye matatizo, mawazo na kwenye bidhaa, hivyo ili waweze kuzipata hawa budi kuanzisha miradi ikiwemo ya biashara watu waende wakanunue watakavyo kuwa wanauza.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo Paschal Masele aliwakumbusha vijana hao juu ya kuzibaini fursa zilizopo Itigi na kuzichangamkia na sio kusubiria wageni wazipate na wao kubakia kuwa vibarua.

Masele alisema kuwa zipo faida nyingi sana za kuzitumia fursa hasa pale wanapokuja wageni kutoka mbali ila pia kuna athari hasi zinazoweza kusababishwa na wageni wakati wa utafutaji ambapo alizitaja baadhi kuwa ni maambukizi ya magonjwa, unyanyasaji wa kijinsia na wizi ambapo aliwataka vijana wa Itigi kuzitazama fursa hizo kwa jicho la tatu ili wanufaike nazo na sio kuangamia.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo Jesca Malya akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema yamewafungua macho kwani walikuwa hawajui chochote kuhusu kupanga babati, kuweka akiba na kuchangamkia fursa lukuki zilizopo wilayani humo kikiwepo kilimo cha alizeti ambapo alimshukuru mratibu wa mafunzo hayo Saimon Sirilo na Mwezeshaji Paschal Masele.


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: