Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja.
Na Amina Hezron,Morogoro
KATIKA kuhakikisha wanawake na vijana wanakuwa na uwezo wa kimamlaka katika usimamizi shirikishi wa misitu na rasilimali za misitu Shirika la kuhifadhi Misitu Asili Tanzania (TFCG) kwakushirikiana na Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wamefanya mafunzo kwa mashirika yote yanayojihusisha na usimamizi shirikishi wa misitu ili kuona jinsi gani wanaweza kuhusisha maswala ya kijinsia katika maswala ya usimamizi ushirikishi wa misitu nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari Afisa Kujengea Uwezo kutoka katika Shirika la kuhifadhi Misitu Asili Tanzania Simon Lugazo ameeleza kuwa tafiti ambazo zilifanyika za kuangalia maswala ya kijinsia yalivyo kwenye vijiji zinaonesha kuzaa matunda ambapo utekelezaji na matokeo unaonyesha hivyo kupitia mabadiliko yaliyopo kwa sasa.
“Ukiangalia umiliki wa ardhi zamani kulikuwa na changamoto wababa tu ndo walikuwa wanamiliki ardhi kupitia hati za kimila lakini kwasasa kuna wamama wengi ambao wamejitokeza na wanaweza kumiliki mamlaka ya maamuzi ilikuwa ni hafifu sana ambapo kwa sasa kuna mabadiliko makubwa sana tunaona wamama na vijana wanachukua nafasi wanaweza kuongea kujieleza na kuhoji“, alisema Bi Kateta.
Kwa upande wake Mtafiti msaidizi kutoka katika kituo cha Stadi za Taaluma za Kijinsia kutoka katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Emmanuel Mroto amesema kuwa matokeo ya tafiti yanaonyesha kuwa Wananchi wamekuwa na muamko katika utunzaji wa misitu na wanaona faida ya kuwa na misitu katika maeneo yao.
“Wengi wameongeza vipato vyao wakiwemo wakina mama na wakina baba lakini pia imetengeneza baadhi ya ajira ambazo hazikuwepo hapo awali mfano mama ntilie kuwapikia wanaopasua mbao au wachoma mkaa pamoja na uanzishwaji wa vingi vinavyowahusisha wakina mama ambavyo vimewasaidia kuwa na uwezo wa kuhimili mahitaji yao muhimu hivyo kuna muamko mkubwa wa kiuchumi ambao jamii zilizolengwa zimeweza kunufaika “, alisema Bw Mroto.
Kwa upande wake Afisa Mradi Msaidizi kutoka Jumuiko la Maliasili Tanzania Fadhila Kateta amesema kuwa Jumuiko huwa linawaanzishia wanawake bustani ndogondo za kupanda miti mbogamboga na matunda ili kuhakikisha anaweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yanaonekana kuwaathiri zaidi kwa upande wao.
“Tumejikita sana katika kuwajengea wanawake uwezo katika kumiliki kutumia na Kudhibiti ardhi ambapo atakuwa na uwezo wa kuitolea maamuzi kama vile mtu wa mwisho waardhi hiyo ambayo anauwezo wa kuuza ama kununua kama vile afanyavyo mwanaume“, alieleza Bi Kateta.
Aidha TFCG kupitia mradi huo imeona haja kuongeza nguvu ya kuwajengea uwezo na wababa pia ili wote waende pamoja katika usimamizi wa misitu .
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika mkoani Morogoro ambapo mashirika hayo yamepata mafunzo ili wakaweze kutoa ujumbe huo unaohusisha maswala ya kijinsia kwa jamii na na kuona namna gani mradi huo unaweza ukasaidia kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya misitu.
Post A Comment: