Serikali inatambua na kuthamini umuhimu na mchango mkubwa wa wauguzi katika jamii na kwamba ndio kada ya afya ambayo watumishi wake wanatumia muda mrefu kuhudumia mgonjwa na hivyo imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zinazoigusa kada hiyo.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu Mh. Dorothy Gwajima ambaye alimuwakilisha Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa katika kilele cha siku ya wauguzi duniani kilichofanyika Mei 12 katika viwanja vya Chuo Cha Ushirika Mkoani Kilimanjaro.


“Nimesikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo suala la kuchelewa kwa muundo wa utumishi wa maendeleo ya kada ya Uuguzi na Ukunga na kutotambua wauguzi wenye stashahada ya juu na wenye shahada ya uzamili (Wauguzi Bingwa), kutozingatia kianzia cha mshahara kwa wauguzi wenye shahada ya kwanza ukilinganisha na muda wa masomo hivyo basi, naagiza Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora pamoja na Waziri wa Afya kupata ufumbuzi wa jambo hili kwa haraka” amesema Dkt. Gwajima



Kuhusu suala la muundo wa utawala katika sekta ya Afya kuongozwa na kada moja Mh. Majaliwa ameagiza Waziri mwenye dhamana ya Afya kulitatua kwa kubadilisha miongozo ili kuwa na muundo shirikishi kama ilivyo kwa nchi zingine. Kwa masuala haya mawili ya miundo nitaomba nipate taarifa ya utekelezaji wake kabla ya kuhitimishwa kwa Bunge la Bajeti kwani masuala haya nilishayatolea maelekezo mwaka 2017 tukiwa Mkoani Lindi;



“Pia kuna suala la ubora wa vyuo vya ukunga na uuguzi kutiliwa shaka kuhusu ubora wa elimu inayotolewa, taaluma hii ni nyeti hivyo ninaagiza Waziri wa Afya akae na Waziri wa Elimu kwa kushirikiana na wana taaluma ili kuona namna ya kuimarisha usimamizi wa vyuo hivyo pia mabaraza ya kitaaluma yasimamie ubora wa vyuo, waalimu na wakufunzi.


Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameitaka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora kuzingatia uwiano wa ajira na kuwa na Maafisa Wauguzi wa kutosha ili kuweza kuinua ubora wa huduma ya afya. 


Naye Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Molleli akitoa salamu za Wizara kwa niaba ya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa wizara iko pamoja na wauguzi kuhakikisha inatatua changamoto mbalimbali ili kuboresha utoaji wa huduma katika kutekeleza majukumu yao sehemu zao za kazi.


“Wauguzi hawa ni Asilimia 60 ya watumishi wote wa afya na wao ndio wanaofanya kazi kubwa kwa asilimia 80 katika hospitali zetu nchini hivyo mafanikio tulionayo katika sektaya afya nikutokana utoaji huduma mzuri wa wauguzi hawa

‘, ameeleza Dkt. Molleli.


Awali akisoma Risala ya Chama Cha Wauguzi Tanzania (TANNA), Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Sebastian Luziga alisema kuwa kada za Uuguzi na Ukunga zinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Muundo wa Utumishi kutotambua wauguzi bingwa, muundo wa utawala katika sekta ya Afya kuongozwa na kada moja, pamoja na maslahi madogo kwa watumishi wa shahada wa kada hiyo licha ya kutumia miaka minne darasani na mmoja katika mafunzo.


Siku ya Uuguzi duniani huadhimishwa kila tarehe 12 Mei, mwaka huu imefanyika katika viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi na ilibeba kauli mbiu isemayo “wauguzi: sauti inayoongoza, wekeza kwenye uuguzi na heshimu haki kwa manufaa ya afya kwa wote”, na imehudhuriwa na wauguzi kutoka sehemu mbalimbali nchini .

Share To:

Post A Comment: