Na Dotto Mwaibale, Singida
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida wametakiwa kutoridhika na Sh.Bilioni 1.5 zinazokusanywa kwa mwaka badala yake waongeze jitihada za kusimamia ukusanyaji ili kuongezeka mapato.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo James Mkwega katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani cha robo ya tatu kilichoketi wilayani humo leo.
Mkwega alisema uhitaji wa bajeti yao ni mkubwa mno kuliko makusanyo hayo hivyo wasibweteke wakidhani ni fedha nyingi kwani zipo halmashauri zingine wanakusanya mapato zaidi ya Sh. Bilioni 5 hadi 30 akitolea mfano Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam na kueleza kuwa hata atapokuwa kwenye vikao vya Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) huwa anachagua wenzake wa kukaa nao wanaolingana katika ukusanyaji wa mapato.
“Ni lazima tukusanye mapato na vyanzo vyetu vipo kwenye maeneo yenu madiwani tusikubali yakatoroshwa na kila unapokubali yatoroshwe unajiibia maendeleo kwenye kata yako hivyo kila mmoja akijihakikishia kulisimamia jambo ili kwa kukaa kwenye mageti kujiridhidha kama mazao yanayosafirishwa kama yamekatiwa ushuru hasa ya vitunguu na mengine itasaidia kuiongezea mapato halmashauri yetu” alisema Mkwega.
Alisema mapato hayo ndiyo yanayoisaidia halmashauri kujenga vituo vya Afya, Zahanati na miradi mingine ya maendeleo.
Mkwega aliwaomba madiwani waliopo kwenye mageti makubwa kusaidia kudhibiti upotefu wa mapato hayo hasa katika maeneo ya Iguguno, Ibaga, Singa, kidalafa na sehemu zingine.
Aidha Mkwega aliwahimiza viongozi wa vijiji na vitongoji na kata kusimamia ukusanyaji wa mapato yanayotokana na madini ya mchanga kwa kuwaomba Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kushirikiana na vijiji husika unapochimbwa mchanga huo au vifusi kwa ajili ya kulipa ushuru ambao ni uti wa mapato katika halmashauri hiyo.
Akizungumzia kuhusu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Mkwega aliwaomba waratibu wa zoezi hilo kuweka nguvu ya kutoa elimu kwa wananchi wa kabila la Waazabe ambao wapo katika wilaya hiyo ambapo iwapo hawatachukua hatua za makusudi kulingana na mazingira wanayoishi wanaweza wasipate takwimu halisi na kujikuta wakikwama.
Hata hivyo Mratibu wa zoezi hilo wilayani humo Daniel Tesha alimuondoa wasiwasi kwa kumueleza kuwa umewekwa utaratibu mzuri kwa wananchi hao kwa ajili ya kushiriki zoezi hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo AsiaMessos aliwahimiza wasimamizi wa zoezi la Anwani za Makazi na Postikodi kuhakikisha linakamilika kwa wakati ndani ya muda uliopangwa kwani linafanyika ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo Lameck Mtungi alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mpango wa kuutangaza utalii wanchi yetu kupitia Filamu ya Royal Tour Tanzania ambayo ilizinduliwa nchini Marekani huku akisisitiza kuwa huwezi kufanya biashara bila ya kujitangaza.
Mbunge wa Iramba Mashariki Francis Isack aliiomba halmashauri hiyo kuandika andiko la kuomba ujenzi wa soko la kawaida na la vitunguu litakaloisaidia kupata mapato ambapo pia aliwapongeza madiwani kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia miradi ya maendeleo.
Katika baraza hilo madiwani walipata fursa ya kuuliza maswali ya papo kwa papo na kujibiwa ambapo pia wenyeviti wa kamati mbalimbali walitoa taarifa ya maeneo wanayoyasimamia na kuyajadili kwa pamoja.
Aidha baadhi ya madiwani walimuunga mkono Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Kizigo kwa kuwaomba waratibu wa zoezi la Sensa ya watu na makazi kuwahimiza watendaji wa vijiji na vitongoji kutangaza nafasi za kuomba ajira ya muda ya ukalani na usimamizi wa zoezi hilo huku wakitoakipaumbele kwa vijana wenye sifa wa wilaya hiyo badala ya kuwachukua kutoka nje ya wilaya hiyo.
Post A Comment: