Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akiwasilisha mada kuhusiana na Sensa ya Makazi wakati wa Kikao cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini mkoani Tanga tarehe 12 Mei 2022. Sehemu ya washiriki wa Kikao cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinachoendelea mkoani Tanga tarehe 12 Mei 2022. Kamisaa wa Sensa 2022 ambaye ni Spika wa Bunge Mstaafu Anna Makinda akiwasilisha Mada ya Sensa ya Watu na Makazi Kikao cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinachoendelea mkoani Tanga tarehe 12 Mei 2022.\

Sehemu ya Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wakifuatilia mada iliyokuwa ikiwasilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi (Hayupo Pichani ) wakati wa kikao cha Maafisa Habari kinachoendelea mkoani Tanga tarehe 12 Mei 2022.

*******************

Na Munir Shemweta, WANMM TANGA

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amewataka maafisa Habari na Mawasiliano Serikalini kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa sensa ya Makazi na watu imayotarajia kufanyika Agosti 2022.

Dkt Kijazi alisema hayo mkoani Tanga tarehe 12 Mei 2022 wakati akiwasilisha mada kuhusiana na Sensa ya Makazi kwenye kikao cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinachoendelea mkoani Tanga.

"Ninyi Maafisa Habari mnatakiwa kuelimisha wananchi umuhimu wa taarifa za majengo, na ni kwanini ifanyike wakati huu" alisema Dkt Kijazi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ni vizuri Maafisa Habari wakashiriki vyema katika zoezi hilo kwa kutoa elimu sambamba na kubainisha changamoto na kutoa mrejesho hata kabla ya kuanza kwa sensa ya makazi.

DKt Kijazi alisema, takwimu zitakazopatikana wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi zitaisadia serikali kupanga na kutekeleza mipango yake itakayoleta mabadiliko katika maendeleo ya kiuchumi.

" Naomba nitoe rai kwa wananchi, waiamini serikali yao kwa kuwa zoezi hili la sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga kutekeleza mipango ya maendeleo itakayoleta mabadiliko katika uchumi vinginevyo hatutapata takwimu sahihi" alisema Dkt Kijazi.

Aidha, alieleza kuwa, lengo la sensa ya watu na makazi pia ni kuiwezesha serikali kuwa na benki ya taarifa za makazi sambamba na kuhakikisha inakuwa na mikakati ya kujua makazi na kujua miji na vifaa vilivyotumika.

"Kama nchi lazima tuzingatia mikakati kulingana na takwimu zilizopo na hii ni Sensa ya kwanza ya makazi" alisema Dkt Kijazi.

Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 Anna Makinda alisema, upo mkakati wa elimu na uhamasishaji kuhusiana na sensa na Maafisa Habari wa Serikali wanalo jukumu la kuhamasisha umuhimu wa sensa.

"Kila aliyekuwa serikalini lazima azungumzie sensa na maafisa habari ndiyo wenyewe na mkasaidie kuhamasisha hasa katika mitandao ya kijamii kwa kuwa wanaosoma zaidi mitandao ni vijana" alisema Makinda.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: