Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Arusha kuhusu usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya TASAF inayotolewa na Serikali wakati wa Kikao Kazi chake na Viongozi hao leo jijini Arusha.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Deogratius Ndejembi amewataka Waratibu wa TASAF kuwasilisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) idadi ya miradi ya TASAF iliyoibuliwa katika maeneo yao na thamani ya fedha inayotumika katika kutekeleza miradi hiyo kwa ajili ya ufuatiliaji ili fedha zilizotolewa zitumike kama ilivyokusudiwa kwa maendeleo ya taifa.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo jijini Arusha wakati wa kikao kazi chake na Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Arusha, Wakurugenzi, Waratibu wa TASAF, Wahasibu wa TASAF na Maafisi Ufuatiliaji kilicholenga kuhimiza usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya TASAF mkoani Arusha.
Amesema TAKUKURU ni lazima washirikishwe ili kujua namna fedha hizi zinavyotumika, hivyo ni lazima kwa wanaohusika na fedha hizi wawe wazalendo kwa maslahi ya taifa lao na thamani halisi ya fedha ionekene kwenye miradi iliyotekelezwa na kuongeza kwa yeyote atakayeleta mzaha atachukuliwa hatua.
Amesema shilingi bilioni 3 zimetolewa katika Mkoa wa Arusha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya TASAF, hivyo amewataka Viongozi na Watendaji wa mkoa huo kuzisimamia kikamilifu ili malengo yaliyowekwa ya wananchi kunufaika na miradi hii ifikiwe na pia mikoa ambayo haikupata fedha hizo iweze kunufaika.
“Lengo lililonileta hapa leo ni kuhusu usimamizi wa hizi shilingi bilioni 3 zilizoletwa na Serikali katika mkoa huu, nimekuja kuona ni namna gani mtazitumia ili kutekeleza miradi ya maendeleo nchini,”Ndejembi amesisitiza.
Aidha,Ndejembi amesema miradi ambayo wananchi wanachangia nguvu zao katika kuiendeleza iwekwe wazi ili kutofautisha gharama ambazo Serikali imetoa na mchango wa wananchi katika miradi hiyo.
Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, katika kuibua miradi ni vizuri kuangalia mahitaji ya wananchi katika eneo husika na endapo hitaji limeshatekelezwa basi ni vema kuangalia hitaji lingine kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
“Kama hitaji lilikuwa ni kujenga madarasa, na tayari yameshajengwa, basi tuangalie mahitaji mengine ya wananchi, unaweza kubadili mradi kwa kufuata taratibu, tuwasaidie wananchi kuibua miradi ambayo ni endelevu,”
Sanjari na hayo, Mhe. Ndejembi amewataka Waratibu hao wa TASAF kuhakikisha miradi yote iliyoibuliwa iwe imekamilika ifikapo tarehe 30 Mei, 2022.
Mikoa mitano ambayo ni Geita, Mwanza, Simiyu, Arusha na Njombe ndiyo iliyonufaika na fedha za miradi ya TASAF Awamu ya Nne iliyotolewa kwa ajili ya ukarabati wa vyumba na madarasa, mabweni, zahanati, vituo vya afya, nyumba za watumishi wa vituo vya afya na walimu, ujenzi wa ukarabati wa vivuko, barabara za vijijini na vyanzo vya maji.
Post A Comment: