Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akiwa na wataalamu na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua mwenendo wa utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amemuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima kuhakikisha anawachukulia hatua wale watakaobainika kukwamisha utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi katika Mkoa huo
Akizungumza leo Jumatatu tarehe 11 Aprili, 2022 jijini Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua mwenendo wa utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Waziri Nape ameonesha kutokuridhishwa na kasi ya utekelezaji katika Mkoa huo unaoshika nafasi ya pili kutoka mwisho
“Hili la Operesheni ya Anwani za Makazi ni jambo letu sote, tuone shida ya kuwa mkiani, wanaotukwamisha washughulikiwe na kama kuna shida kwenye utekelezaji tuelezane tutatue kwa pamoja”, Amezungumza Waziri huyo
Waziri Nape amesisitiza kuwa uwekaji wa Anwani za Makazi sio zoezi la kawaida ni operesheni maalum iliyotangazwa na Rais, ambapo kukamilika kwake kutarahisisha kufanyika kwa sensa ya watu na makazi na ufikishaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Adam Malima amekiri utekelezaji wa Operesheni hiyo bado haujaanza katika halmashauri tatu za Mkoa huo, ambazo ni halmashauri ya Korogwe mji, Korogwe vijijini na Kilindi kutokana na changamoto za kiutendaji
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Mfumo wa kielektoniki unaoingiza taarifa za wakazi na makazi unafanya kazi vizuri, na Wizara hiyo ipo tayari kutoa wataalamu kwenda kuongeza nguvu kwenye mkoa au halmashauri yeyote ambayo ina uhitaji.
Post A Comment: