Julieth Ngarabali, Pwani
Ulinzi wa mtoto dhidi ya aina zote za vitendo vya kikatili imeelezwa ni jukumu la jamii nzima ikiwemo mlezi na mzazi mmoja mmoja kwa nafasi yake katika ngazi ya familia pamoja na Serikali kwa ujumla
Vitendo hivyo vya kikatili ni pamoja na ubakaji, ndoa za utotoni, ukatili wa kudhuru mwili, kutelekezwa kwa watoto,ukeketaji pamoja na usafirishaji haramu .
Hayo yameelezwa na wakazi wa kata ya Mualakani walipokua wakizungumzia nafasi ya wazazi, jamii na Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata ulinzi dhidi ya aina zote za vitendo vya kikatili.
Grace Marwa mkazi wa Jamaika Kibaha amesema anavyotambua ushirikiano katika malezi ya mtoto kati ya wazazi, walezi pamoja na jamii unahitajika kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha usalama wa mtoto wakati wowote iwe nyumbani, mtaani na anapokua shule.
" kwani unafikiri watu hawajui umuhimu wa kumlinda mtoto? Wanajua sana maana tangu mimba kliniki tunaelekezwa, sema tuu hali ya maisha ni ngumu unakuta mama au baba anatoka alfajiri kuwahi kuuza mboga sokoni apate senti ya sembe na kule nyumbani kamuacha mtoto wa miezi tisa na mwenzake wa miaka minne wanaleana si salama ila ndio ilivyo"amesema Grace.
Bosco Mfundo mkazi wa Picha ya Ndege amesema sehemu nyingine ya muhimu ni ushirikiano na mahusiano ya karibu kati ya mwalimu na mzazi ili kuhakikisha mienendo ya mtoto darasani, mtaani hadi nyumbani.
Diwani kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi amesema "ni vema ieleweke kwamba mzazi, jamii na Serikali tukishirikiana hatuwezi hata siku moja kuwaona watoto wakiwa mitaani wanazurura muda ambao wanatakiwa kuwa shuleni nasi tubaki kimya."
Vivian Laizer mwalimu wa shue binafsi ya Tumaini amesema ulinzi uanze katika ngazi ya familia mpaka shuleni ambapo mawasiliano ya mara kwa mara kati ya pande hizo unapaswa uwepo na sio kuachiwa mwalimu pekee.
" Utawakuta watu wazima wanawake na wanaume wamekaa vibarazani katika nyumba zao wakitia soga na kuongea masuala yao ya kiutu-uzima ikiwemo kutamka matusi mbele za watoto pasipo kuwafukuza, katika familia kupigana na kutoleana lugha chafu mbele za watoto si jambo jema tunawangamiza hawa viumbe"amesema Vivian
Mratibu wa magonjwa ya kifua kikuu (TB ) mkoa wa Pwani Dk. Aden Mpangile amebainisha kuwa mzazi ndiye mwenye wajibu zaidi kujenga maadili na ulinzi wa mtoto tangu akiwa na umri wa miaka sifuri (tumboni)
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri hivi karibun katika maadhimisho ya siku ya sheria amesema Serikali inadhamini watoto na kuwalinda na ndio maana hata wale wanaoshtakiwa Mahakamani kesi zao haziendeshwi hadharani kama zingine.
Wakati huo huo kupitia programu Jumuishi ya Taifa ya malezi ,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT -MMMAM ) 2021/2022 -2025 /20 26 kwenye eneo la Ulinzi na Usalama uelimishaji jamii na juhudi za makusudi za sekta mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika upatikanaji wa huduma za uandikishaji watoto kupitia afua mbalimbali zimechangia kuongezeka kwa uandikishaji wa watoto kutoka asilimia 26 mwaka 2016 mpaka 49 mwaka 2020
Aidha mpango huo Serikali wa PJT - MMMAM katika vitendo vya ukatili wa watoto kuna upungufu wa utoaji taarifa za kesi za unyanyasaji na utelekezaji watoto kuanzia miaka 0 mpaka minane ambapo kwa utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia katika mkoa wa Katavi umeonyesha asilimia 18 ya wazazi wenye watoto chini ya miaka mitatu kuwapiga vibao watoto wao.
Post A Comment: