.Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kushoto)
akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (kulia) namna
Wizara yake ilivyojipanga kuwainua wavuvi wa Ziwa Tanganyika muda mfupi
baada ya kufika ofisini kwa Mkuu wa mkoa huyo leo (08.04.2022).Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya kimataifa ya kusafirisha mizigo ya DHL,
Bw. Paulo Makolosi (kulia) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Abdalla Ulega jinsi kampuni hiyo inavyofanya kazi zake ikiwa ni
muda mfupi kabla ya makabidhiano ya Boti ya doria ya uvuvi yaliyofanyika
leo (08.04.2022) kwenye Fukwe za Hoteli ya Hiltop mkoani Kigoma.Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya kimataifa ya kusafirisha
mizigo ya DHL, Bw. Paulo Makolosi (kushoto) akimkabidhi Naibu waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalla Ulega boti ya doria ya Uvuvi kwenye hafla
iliyofanyika leo (08.04.2022) kwenye Fukwe za Hoteli ya Hiltop mkoani
Kigoma. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt.
Rashid Tamatamah.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega
amesema kuwa Wizara yake itahakikisha inalinda rasilimali za Uvuvi
wakati wote ili ziendelee kuwa mkombozi kwa wananchi wanaozunguka vyanzo
mbalimbali vya maji ya asili vilivyopo hapa nchini.
Mhe.
Ulega ameyasema hayo leo (08.04.2022) wakati wa hafla ya makabidhiano
ya boti ya doria ya uvuvi iliyotolewa na Kampuni ya kimataifa
usafirishaji wa mizigo ya DHL tukio lililofanyika kwenye ufukwe wa hotel
ya Hiltop mkoani Kigoma.
"Kwa
sasa tuna kikosi cha wataalam ambacho ni kitengo cha kulinda rasilimali
zilizopo katika Ziwa Tanganyika na mtu anaweza asielewe umuhimu wa kazi
inayofanyika lakini ni lazima tutekeleze jukumu hili ili kuhakikisha
rasilimali hizi zinakinufaisha kizazi kilichopo na kijacho na ninatambua
suala hili sio jepesi kwetu kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao
wamekuwa wakinufaika kwa kutumia njia zisizo halali kwenye shughuli zao
za Uvuvi" Amesisitiza Ulega.
Mhe.
Ulega amesema kuwa Wizara ina mpango wa kukiongezea zaidi uwezo kikosi
kazi hicho ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ambapo
alibainisha kuwa wameshawasilisha mawazo ya kukiongezea nguvu kikosi
hicho kwa mamlaka za juu ili kiweze kuwa na vitendea kazi vya kisasa na
kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu
yao.
"Hawa wanaobeza
kazi ya ulinzi wa Rasilimali hizi siku wakiamka na kukuta hakuna samaki
watakosa shughuli ya kufanya na watatuuliza wataalam tulikuwa tunafanya
shughuli gani hivyo naomba muendelee na shughuli yenu ya ulinzi wa
rasilimali hizi ili tuendelee kuunga mkono kampeni ya Mhe. Rais Samia
Suluhu Hassan ya Uchumi wa buluu ambao utamnufaisha kila mwananchi na
Taifa kwa ujumla" Amesema Ulega.
Mhe.
Ulega ameipongeza kampuni hiyo kwa kutoa boti hiyo ya ulinzi wa
rasilimali za Uvuvi ambapo mbali na kutekeleza jukumu hilo la msingi
amewataka wataalam watakaoisimamia kuhakikisha inatumika kutoa msaada
hata kwa wavuvi watakaokumbana na changamoto mbalimbali wakiwa kwenye
shughuli zao majini.
Mhe.
Ulega ameishukuru kampuni ya DHL kwa msaada wa boti hiyo ambayo
inafanya idadi ya jumla ya boti za doria zinazofanya kazi kwa upande wa
Ziwa Tanganyika kuwa 10 huku nyingine ya 11 itakayokuwa ukanda wa Kigoma
ikitarajiwa kutolewa na Serikali kabla ya Mwezi Mei mwaka huu.
"Sisi
pale Wizarani tumekubaliana Dagaa la Kigoma liwe moja ya mazao yetu ya
kimkakati na DHL wameiona hiyo fursa ambapo wao wameamua kujikita kwenye
kuongeza thamani ya bidhaa hiyo mpaka inafika kwa mlaji huko nje ya
nchi na niwaombe wadau wengine wenye nia ya kutumia fursa zilizopo Ziwa
Tanganyika na kwingineko waje kwa sababu Serikali yetu inawakaribisha
sana wawekezaji wenye nia ya kukuza uchumi wa mwananchi na kuongeza pato
la Taifa " Amesema Ulega.
Akibainisha
umuhimu wa boti hiyo kwa upande wa shughuli za Uvuvi, Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo anayeshughulikia sekta ya Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah
amesema kuwa itasaidia kuwezesha uvunaji endelevu wa rasilimali za uvuvi
katika Ziwa Tanganyika.
"Kwa
mujibu wa taarifa ya takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2018
inaonesha kuwa Ziwa Tanganyika linaajiri moja kwa moja wavuvi 26612
ambao hutumia vyombo vya uvuvi 11506 na zaidi ya watu laki 7 hunufaika
na shughuli zinazofanyika upande wa Ziwa Tanganyika" Amesema Dkt.
Tamatamah.
Mbali na boti
hiyo Dkt. Tamatamah amesema kuwa boti nyingine 9 zinazofanya kazi kwa
upande wa Ziwa Tanganyika zipo katika vituo vya Kipili, Kasanga, Ikola
na moja ikiwa katika kituo cha Buhingu.
Kwa
upande wake Mkurugenzi mkazi wa kampuni hiyo hapa nchini Bw. Paulo
Makolosi amesema kuwa wakati wanafika mkoani Kigoma walikuta
wasafirishaji wa dagaa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo
upoteaji wa mizigo yao ikiwa njiani, kupotea kwa ubora wa mazao hayo na
kutokuwa na vifungashio bora vya kusafirishia mizigo yao.
"Dagaa
walikuwa wakiuzwa kwenye mifuko maarufu kama "shangazi kaja" hivyo
tukachukua jukumu la kulialika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo
lilitoa mafunzo zaidi ya mara sita hapa Kigoma ambapo tuligharamia kila
kitu ili kuhakikisha wafanyabiashara wa Kigoma wanabadilika na kufanya
shughuli zao kwa kuzingatia viwango stahiki" Amesema Makolosi.
Ameongeza
kuwa baada ya kumaliza mafunzo hayo, waliamua kutoa msaada wa
vifungashio ambavyo vitasaidia kuzifanya bidhaa hizo zinazosafirishwa
kutopoteza ubora wake hata zikikaa kwa muda mrefu.
Katika
kuhakikisha sekta ya Uvuvi inaendelea kukua, Serikali ya awamu ya Sita
chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza kwenye miundombinu ya masoko
na mialo ya kisasa ya kupokelea samaki ukiwemo mwalo wa Kibirizi uliopo
Kigoma, soko la Kasanga lililopo Sumbawanga, mwalo wa Ikola uliopo
Katavi na soko la Kirando lililopo mkoani Rukwa.
Post A Comment: