WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka taasisi za fedha kubuni mikakati na mbinu zitakazowezesha watanzania wengi zaidi kupata huduma rasmi za kibenki kwa gharama nafuu ili waweze kujiongezea kipato na kujikwamua na umasikini.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Aprili 11, 2022) katika hafla ya huduma ya Teleza Kidijitali inayotolewa na Benki ya NMB, iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Morena jijini Dodoma. Amezishauri taasisi nyingine za kifedha ziige utoaji wa huduma kwa njia hiyo.
Waziri Mkuu amesema kuwa taasisi hizo hazina budi kuiunga mkono Serikali kwa kubuni mikakati mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kukuza uchumi sambamba na kubuni masuluhisho rahisi kwa watumiaji wa kawaida.
Amesema benki nchini hazina budi kubuni zaidi namna ya kutafuta masuluhusho yaliyo katika sekta za kifedha. “Hongereni NMB kwa ubunifu huu ambao utavutia makundi yote ya kijamii, huduma hii itawezesha wateja wenu kupata huduma ya mikopo kiganjani.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema amevutiwa na huduma hizo ikiwemo ya MshikoFasta ambayo inakwenda kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa haraka kwa mama lishe na baba lishe, bodaboda, wafanya biashara wadogo na wananchi wote wa kawaida.
Amesema Wakati Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza na wamachinga hivi karibuni aliziasa taasisi za fedha kulizingatia kundi hilo muhimu na zihakikishe huduma za kifedha zinakuwa rafiki kwao, hivyo ameipongeza NMB kwa utekelezaji huo.
“Ninaipongeza NMB kwa kuja na suluhisho hili, naamini asilimia kubwa ya Watanzania watanufaika sana na huduma hii katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana na changamoto ya ajira kwa vijana. Hii ni fursa ya vijana kujipatia mitaji.”
Amesema huduma hiyo ya mikopo ya kidigitali inakwenda kumaliza kabisa tatizo la ugumu wa kupata mikopo. “Hii ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya kibenki Tanzania. Tukio hili linapeleka ujumbe kwa Watanzania wa kuwataka wasihangaike kupata mikopo ya kuanzisha biashara zao kwa kuwa fedha ipo NMB.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali kwa upande wake inaendelea kuimarisha usalama wa mtandao kwa kuwajengea uwezo watalaamu wa TEHAMA pamoja na kujenga mazingira wezeshi ya kisera, sheria, mifumo, miundombinu na kuhakikisha uwepo wa wataalamu hao kwenye nyanja zote muhimu za ubobezi.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo katika hatua za awali za maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali pamoja na Mkakati wa Taifa wa Brodibandi utakaowezesha asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za intaneti yenye kasi ifikapo 2025.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema kuwa uzinduzi wa Huduma ya Teleza Kidijitali ni ishara kwamba benki hiyo imejipanga kupanua wigo wa huduma kote nchini “ninaamini kuwa huduma zitakuwa za gharama nafuu ili kuvutia wengi zaidi kujiunga na huduma hizi”
Amesema kuwa maboresho yaliyofanyika katika Sekta ya Fedha yameleta matokeo chanya ambapo mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuimarika na kuongezeka kutoka shilingi trilioni 20.31 mwaka 2020 hadi kufikia shilingi trilioni 22.34 mwaka 2021 sawa na ukuaji wa asilimia 10 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.1 mwaka 2020.
Aidha, katika mwaka 2021, amana za benki za biashara ziliendelea kuongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 26.81 ikilinganishwa na shilingi trilioni 23.81 mwaka 2020, sawa na ukuaji wa asilimia 13.0. Kati ya amana hizo, sekta binafsi iilifikia shilingi trilioni 26.39, sawa na asilimia 98.4 ya amana zote.
Kwa upande, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Prof. Florence Luoga amesema malengo ya BOT ni kuhakikisha kuwa ifike wakati kila Mtanzania anapata huduma jumuishi za kifedha za uhakika chini ya kilomita 15.
Amesema uzinduzi wa huduma hii unakidhi malengo ya BOT ya kuhakikisha mabenki yanajenga uwezo wa kuwafikia wananchi pale walipo na kwa namna rafiki inayoweza kuongeza ari kwa wananchi kutumia huduma za kifedha “Ninaamini benki nyingine zitaiga mfano huu”
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema lengo la kuanzisha huduma hiyo ya Teleza Kidijitali ni kuendelea kuchagiza ukuaji wa teknolojia kwa sababu huduma hizo zinaenda kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa jamii.
Pia, Afisa Mtendaji huo amesema mbali na huduma hiyo, pia benki ya NMB imetenga shilingi bilioni 200 kwajili ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu machinga ili kuwawezesha kukuza mitaji yao.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede amesema malengo makuu wa benki ya NMB ni kuwafikia Watanzania kwa kasi na ubora wa huduma. uzinduzi wa programu ya Teleza Kidijitali ni utekelezaji wa mpango huo.
Aidha, aliwataka wateja wa benki hiyo kuitumia kwa busara huduma hiyo na watumishi wao watakuwa tayari kutoa ushirikiano ili waendelee kunufaika na mapinduzi makubwa ya kisekta.
Post A Comment: