Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutumia mkaa mbadala (Rafiki Briquettes) utokanao na madini ya makaa ya mawe ili kuchangia utunzaji wa uoto wa asili na kupunguza uharibifu wa mazingira utokanao na ukataji miti.


Elimu hii imetolewa kupitia maonesho yaliyoandaliwa wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha  Mapinduzi uliofanyika Aprili 1, 2022 katika viwanja vilivyopo  Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini DODOMA.


Akiongea kuhusu mpango mkakati  wa STAMICO katika kuutangaza mkaa huo Bw. David Semeo amesema Shirika limejidhatiti kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza ili kufikisha elimu kuhusu Mkaa huu kwa watu mbalimbali.


Amesema mkaa huu umeletwa ili kuleta tija kwa mazingira ya nchi yetu na utumiaji wa mkaa huu  utapunguza kasi ya ukataji miti katika maeneo mengi ya nchi hivyo mkaa huu ni rafiki kwa mazingira, matumizi.


Akiongea wakati alipotembelea banda la STAMICO  Bw. Sixtus Mapunda mjumbe wa Chama Cha Mapinduzi  amesema mkaa huu utaleta tija kwa wananchi endapo utawafikia hadi wananchi wa vijijini. 

"Mkaa huu unaonesha kuleta tija sana kwa wananchi wote hasa wanaotumia nishati ya mkaa wa miti, hivyo ni vyema Shirikia  likajipanga kuzalisha kwa wingi na kuusambaza kwa wananchi"


Naye Dkt. Brighton Gwamagobe ameipongeza STAMICO na kusema kuwa inatakiwa kuhakikisha inapata vyeti vya udhibitisho wa kutokuwepo kwa sumu mbalimbali  ili mkaa huo uweze kutumika kimataifa.


Shirika linaendelea kutoa elimu  ya mkaa wa Rafiki  Briquette kupitia mikutano, makongamano mbalimbali ili kuchochea matumizi ya mkaa huo ambao umetengenezwa kwa ajili ya matumizi ya  kupikia majumbani, mashuleni na maeneo mengine yenye uhitaji wa nishati ya kupikia kama hii.











Share To:

JUSLINE

Post A Comment: