Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda (wa pili) akiwa na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa jengo la Wagonjwa Mahututi (ICU) linalojengwa Hospitali ya Wilaya Kiomboi mkoani Singiga juzi. Kulia ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Kiomboi Abel Mafuru.
Mhandisi wa Wilaya hiyo, Profiri Modaha akitoa maelezo ya ujenzi wa jengo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akizungumzia ujenzi huo wakati wa ukaguzi.
Wajumbe wa kamati hizo wakikagua matengenezo ya barabara ya Old Kiomboi-Kisinda na Doromoni.
Ukaguzi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Tyegelo ukifanyika .
DC Mwenda akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa kituo hicho cha Afya.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Beatrice Mashausi akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akihutubia kwenye mkutano huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
ZAIDI ya Sh.Bilioni 2 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan
katika mwaka mmoja wa uongozi wake zimewawezesha Wanawake wa Tarafa ya Kisisiri iliyopo Wilaya
ya Iramba mkoani hapa kuwatua ndoo za maji baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa
wa maji uliotekelezwa kutokana na fedha hizo.
Kabla ya kutekelezwa kwa mdari huo wanawake hao walikuwa na adha kubwa na kutumia muda mwingi kutembea
umbali mrefu kutafuta maji ya visima vya kuchimba kienyeji huku wakiwa hawana uhakika wa kuyapata maji hayo ambayo hayakuwa salama kwa matumizi ya
kunywa.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda wakati akiwahutubia wananchi wa Tarafa ya Kisiriri kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Didaru baada ya kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo
kumaliza ziara ya siku moja ya kukagua miradi ya maendeleo katika Tarafa hiyo juzi.
Mwenda alisema kamati hizo zilifanya ukaguzi wa miradi hiyo ili kuona
nini kimefanyika katika mwaka mmoja wa uongozi wake Rais Samia Suluhu Hassan
ambaye ametoa fedha nyingi kwa ajili ya
kutekeleza miradi mbalimbali.
Mwenda aliitaja miradi walioitembelea na kuikagua kwa sekta ya elimu
kwa Shule za Msingi kuwa ni ukamilishaji wa darasa moja katika Shule ya Msingi
Kiomboi Hospitali ambapo walipokea Sh.11,363,636.40, ukamilishaji wa darasa
moja Shule ya Msingi Kisimba ambao pia walipokea Sh.11,353,636.36 ambao ujenzi
wake umefikia hatua ya lenta ambao unatekelezwa kwa nguvu ya Wananchi.
Halikadharika Mwenda alitaja miradi mingine kuwa ukamilishaji wa
darasa moja katikaShule ya Msingi Tulya kwa gharama ya 11,363,636.36,
ukamilishaji wa ujenzi wadarasa moja Shule ya Msingi Doromoni kwa kiasi hicho
hicho cha fedha kilichotolewa Shule ya Tulya ambapo jumla ndogo ya miradi hiyo ikiwa ni
Sh.45,454.,545.48.
Akiitaja miradi ya Shule za
Sekondari iliyotekelezwa kuwa ni ujenzi wa chumba kimoja cha darasa Shule ya
Sekondari Kisiriri ambao umetumia Sh.20,000,000, ukamilishaji wa vyumba viwili
vya maabara katika Shule ya Sekondari ya Kisana ambapo walipokea Sh.30,000,000
na ukamilishaji wa vyumba vingine viwili vya maabara katika Shule ya Sekodari
ya New Kiomboi kwa gharama hiyohiyo na kuifanyajumla ndogo kuwa ni Sh.60
Milioni.
Akielezea Sekta ya Afya alisema wamejenga Kituo cha Afya Kisiriri kwa
gharama ya Sh.250,000,000 na kuwa ujenzi wake upo katika hatua ya umaliziaji
jengo la OPD likiwa kwenye hatua za upakaji wa rangi, kuwekwa milango na
madirisha na halikadharika jengo la maabara.
Alitaja mradi mwingine wa sekta ya Afya kuwa ni ujenzi wa Kituo cha
Afya Tyegelo ambao pia walipokea Sh.250,000,000, ujenzi wa choo Zahanati ya
Doromoni ambao unatekelezwa kwa gharama ya Sh.40,000,000, ujenzi wa choo
Zahanati ya Kisana kwa gharama ya Sh.39,950,000 jumla ndogo yake ya ujenzi wa
vyoo hivyo ikiwa ni Sh.79,950,000 huku ujenzi wa Zahanati ya Tutu ukigharimu
Sh. 50,000,000.
Mwenda aliongeza kuwa katika Sekta hiyo ya Afya wanakamilisha ujenzi
wa wodi ya dharura (EMD) katika Hospitali ya Wilaya ambapo wamepokea
Sh.300,000,000, ujenzi wa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kwa gharama ya
Sh.250,000,000 huku jumla yake ndogo ikiwa ni Sh.550,000,000.
Aidha Mwenda akizungumzia Sekta ya barabara alisema wanafanya
matengenezo ya barabara ya Kisiriri-Kisimba kilometa 9.42, Old
Kiomboi-Meli-Walla-Ntwike kilometa 0.9, matengenezo ya kawaida barabara ya
Kitusha-Kisana Kilometa 6.0 na ujenzi wa
mifereji mita 100 kwa gharama ya Sh.126,383,800.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni matengenezo muda maalum barabara ya
Kiomboi-Ruruma-Uwanza kilometa17.4 kwa gharama ya Sh.492,019,500, matengenezo
muda maalum barabara ya Old Kiomboi-Kisimba-Doromoni Kilometa 9 na kufungua
barabara ya Kibigiri Masagi-Kinkungu na kufungua barabara ya Migilango kilometa
5 na na Barabara ya Mwamapuli- Luono ambazo zote kwa pamoja jumla yake kuu ni Sh. 1,295,947,201.
Alisema mradi mwingine walioukagua ni upelekaji wa umeme kwenye kitongoji cha Tutu ambao unatekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya Sh.122,331,420.54 ambao umekamilika kwa asilimia 100.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo Mwenda alisema miradi hiyo
inafanyika ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
Serikali inawajibu wa kuikagua ili kuona kama inatekelezwa kwa viwango vinavyo hitajika.
Mwenda alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo na kuwaomba viongozi ilipo miradi hiyo kuwahamasisha wananchi wao kuitunza.
.Aidha Mwenda aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa vijana wanaoshiriki katika zoezi la anuani za makazi na postikodi linaloendelea nchi nzima kwa kuwaelekeza majina ya mitaa na mambo mengine yanayohitajika na akawaomba kufanya hivyo pia katika zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Ziara hiyo ambayo imeleta ari na mwamko mkubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo kushiriki shughuli za maendeleo baada ya kupokea taarifa ya miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo pia walitumia nafasi hiyo kumpongeza pamoja na mbunge wao Dk.Mwigulu Nchemba kwa kutoa fedha nyingi ilifanyika katika Tarafa za Ndago, Kinampanda, Shelui na Kisiriri zenye jumla ya kata 20 na vijiji 70.
Post A Comment: